Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Hapi: Tunahitaji mpango mkakati kukuza utalii Nyanda za Juu Kusini

65711 Pic+hapi

Sat, 6 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amesema ni muda mwafaka kwa  wadau wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuweka mpango mkakati kuhakikisha wanaongeza idadi ya watalii kwenye vivutio vyake vya kitalii.

Hapi amebainisha hilo leo Julai 5, 2019 mkoani Iringa, Tanzania,  wakati akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya utalii kanda hiyo ukilenga kujadili na kuweka mpango madhubuti wa pamoja katika kukuza na kutangaza sekta ya utalii.

Hapi amesema bado vivutio vilivyopo ukanda wa Nyanda za Juu Kusini havijatangazwa ipasavyo ikilinganishwa na vivutio vya kanda nyingine kama vile kanda ya kaskazini, hivyo ipo sababu kuhakikisha wanashirikiana na wadau wote kukuza utalii na kuwavutia watalii.

Amesema licha ya kanda hiyo kuwa na maeneo makubwa na vivutio vingi vizuri lakini watalii wanaofika na kutembelea hawafiki 50,000 kwa mwaka mzima katika ukanda huo hivyo wana kazi kubwa ya kuifanya ili kuona sekta ya utalii inakuwa na mchango mkubwa kwenye pato la taifa.

 Amesema, “Tumepewa takwimu za idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi zetu huku Kusini kwamba Hifadhi ya Ruaha ambayo ndiyo kubwa kuliko zote barani Afrika inapata watalii kati ya 23,000 na 25,000 kwa mwaka, Hifadhi ya Katavi inapata watalii kati ya 13,000 na 14,000 kwa mwaka huku Kitulo ikiambulia kupata watalii kati ya 500 na 600 kwa mwaka, sasa hii hairidhishi na lazima tutengeneze mpango mkakati kuhakikisha tunakuza utalii wetu.”

Awali, Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi wa Hifadhi za Taifa za Wanyama kutoka Ofisi ya Dodoma, Ahmed Mbugi, amesema katika kutangaza vivutio sio lazima iwe kwenye hifadhi za wanyama kwani kuna watalii wengine wanapenda kuona vitu vya asili vikioneshwa kama vile kuona mauwa, kucheza ngoma za asili.

Pia Soma

Amesema shughuli za kutangaza utalii unahitaji ushirikishwaji wa wadau wengi, hivyo watu wote wanakaribishwa kwenye maeneo ya hifadhi na kufanya uwekezaji wao.

Mbugi amesema utalii ni moja ya sekta za kimkakati na  Serikali imeiweka kwenye mpango wake wa miaka mitano  kama ni sekta muhimu ambazo zitakiwa kuangaliwa kwa ukaribu.

Chanzo: mwananchi.co.tz