Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Geita anusa ubadhirifu fedha za Corona

54e4616f0639bdef20f0ebdced81c498.jpeg RC Geita anusa ubadhirifu fedha za Corona

Sun, 26 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ameunda kamati ya watu 35 kuchunguza tatizo la makadirio ya gharama ya vifaa vya ujenzi (BOQ) kwa madarasa iliyosababisha kuwepo na ziada kubwa katika vifaa.

Senyamule alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari akitoa salamu za Krismasi na Mwaka mpya kwa wananchi wa Geita na kueleza kwamba kamati hiyo ina timu saba na kila timu itakuwa na watu watano.

Alisema kamati hiyo itafanya kazi kwa siku tatu kuanzia Desemba 27 hadi 29 na itatembelea halmashauri zote sita na kwamba Desemba 30 wataandaa taarifa na Desemba 31 watakabidhi taarifa ili maamuzi yafanyike.

“Timu hizo zitafanya kazi na zitatuletea taarifa ya kina ambayo inaenda kutuambia uhalisia wa tatizo hili lilianzia wapi, likafika wapi lakini zaidi sana ukubwa wa tatizo lenyewe na kutushauri nini cha kufanya.”

Senyamule alisema amefikia hatua hiyo baada ya kufanya ziara katika halmashauri ya mji wa Geita na kubaini tatizo la BOQ ni kubwa na limesababisha uwepo wa ziada kubwa ya vifaa vilivyobaki baada ya ujenzi.

“Kuna shule tulikuta saruji imebaki mifuko 340, sasa imebakije na ameshamaliza kujenga, tumeenda kwingine mifuko 126, tumeenda kwingine mifuko 220, tumeenda kwingine mbao 200, kwingine nondo 58.

“Tulichoagiza baada ya kubaini tatizo, vifaa vikae palepale, vihifadhiwe, visiguswe, mpaka tutakapotoa maelekezo na tunaendelea kupokea taarifa zingine kutoka kwa raia wema juu ya ubadhirifu huo. Hofu yetu kubwa ni kwa nini tutumie hela nyingi ya serikali kununua kitu ambacho hakihitajiki?” Alihoji.

Senyamule alisema baada ya kubaini tatizo aliagiza kupata BOQ za wahandisi wa halmashauri zote na kushtushwa na utofauti mkubwa uliopo huku ikizingatiwa ukubwa wa madarasa nchi nzima unafanana.

“Mmoja anasema simenti kwa darasa inahitajika mifuko 70, mwingine anasema mifuko 169, mwingine anasema 101, mwingine anasema 189 sasa yote hayo yameendelea kutushangaza.

“Madarasa si kitu kipya kwetu kujenga, tunajenga madarasa kila siku kwa kutumia nguvu za wananchi, hela za halmashauri na Fedha za Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR) kwa nini tutofautiane hivyo?” Alihoji.

Alibainisha kwamba mbali na kamati hiyo, pia amewaagiza wakurugenzi wote kufanya ufuatiliaji wa tatizo la BOQ kwani huenda ikawa ni hujuma, ubadhirifu, wizi na ufujaji wa fedha za Mradi wa Madarasa kwa Fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya

Covid-19.

Awali akiwa katika ziara ya kukagua miradi hiyo ya madarasa mkuu huyo wa mkoa aliagiza uchunguzi ufanyike juu ya viashiria vya ubadhirifu vinavyoonekana katika miradi ya ujenzi wa madarasa kwa fedha hizo za Covid-19.

Alitoa maagizo hayo juzi akiwa katika ziara ya Halmashauri ya Mji wa Geita kukagua miradi hiyo na kujionea idadi kubwa ya vifaa vya ujenzi wa madarasa maeneo mengi vikiwa vimebakia baada ya ujenzi kukamilika.

Akikagua ujenzi wa madarasa manne ya Shule ya Sekondari ya Shantamine iliyopo Kata ya Mtakuja wilayani Geita, Senyamule alishangaa kuona mifuko ya saruji 340 imebakia.

“Madarasa manne huwezi kubakiwa na saruji mifuko 340, hapo kuna dhamira gani kama sio wizi, nina taarifa kuna shule imezidisha mbao 240, kwa kweli nataka tumjue aliyepelekea hali hii maana ana dhamira mbaya,” alisema.

Akiwa Shule ya Sekondari ya Lukaranga, Kata ya Nyankumbu, Senyamule alishtushwa kuona madarasa manne yamejengwa kwa Sh milioni 80 na wamebakisha zaidi ya mifuko 180 ya saruji na zaidi ya mbao 200.

Aidha, akiwa shule ya Sekondari Bung’wangoko Kata ya Bung’wangoko, Senyamule alishuhudia madarasa manne yamejengwa kwa Sh milioni 80 huku kukiwa na ziada ya mabati 17, nondo 56, mbao 100 na mifuko ya saruji 300.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live