Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Dodoma aonya wauza sukari

Sukari Zanzibar RC Dodoma aonya wauza sukari

Tue, 27 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa onyo kwa wafanyabiashara wa sukari mkoani humo wanaouza kwa bei kubwa badala ya elekezi iliyotolewa na Serikali.

Senyamule ametoa onyo hilo leo Jumatatu Februari 26, 2024 alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye maduka ya mawakala waliopewa kibali cha kuingiza sukari nchini na kujionea hali halisi ya bei zinazotumika kuuza biadhaa hiyo.

Akiwa kwenye duka la Wakala Haidary Gulamali, Senyamule ameagiza sukari hiyo kuuzwa kwa bei elekezi kama Serikali ilivyoagiza ili kila mtu apate.

Amesema sukari hiyo imeingizwa nchini bila kutozwa kodi ya aina yoyote, hivyo inatakiwa kuuzwa kwa bei ya jumla Sh2,800 au chini ya hapo kwa kilo moja na maduka ya rejareja inapaswa kuuzwa Sh3,000 kwa kilo moja.

“Na hapa tumeweka utaratibu, mtu mmoja anatakiwa anunue mifuko mitano tu ili na wengine wapate, lakini baadhi ya wafanyabiashara wanawatuma vijana hata kumi kuja kununua, wanasababisha maeneo mengine yakose sukari na wakati yeye amenunua sukari nyingi zaidi,” amesema Senyamule.

“Lakini niwatahadharishe wale ambao wana mpango wa kuuza sukari kwa bei ya juu maana nimeona hapa bei ya jumla ni Sh2,800 kwa kilo kwa bei ya jumla, lakini kuna wengine wakitoka hapa wanakwenda kuuza kwa Sh5,000 hadi Sh6,000, niwaambie tu tumewakamata wenzenu 17 kwa kosa la kuuza sukari tofauti na bei elekezi, kwa hiyo tutawafuatilia huko mliko na tutawakamata.”

Meneja mauzo kutoka Kampuni ya Haidary Gulamali ambayo imepewa kibali cha kuagiza sukari, Sameer Hussein amesema kampuni hiyo imeagiza tani 58 kutoka Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa ambayo imeisha leo.

“Bado kuna uhitaji mkubwa wa sukari kwa sababu hata hizi tani 58 zilizoingia leo, zimeisha leo na wengine wamekosa kwa hiyo, Serikali iendelee kuongeza jitihada za upatikanaji wa sukari ili iweze kukidhi mahitaji ya wananchi,” amesema Hussein.

Muuzaji wa duka la rejareja, Emmanuel Edwin amesema pamoja na mawakala kupewa kibali cha kuingiza sukari nchini, bado upatikanaji wake ni mgumu.

Amesema kwa mfano walioandika majina Februari 20, mwaka huu, walioenda leo wamekosa.

Wamelazimika kuandika majina tena waone kama wataipata kesho.

Amesema bei elekezi ya sukari iliyotolewa na Serikali kwa mfuko wa sukari wa kilo 50 ni Sh140,000, lakini hao mawakala wanauza bei ya juu hadi Sh150,000, hivyo wanashindwa kuuza kilo Sh3,000 kwenye maduka yao kwa sababu haina faida.

“Siwezi kununua mfuko wa kilo 50 kwa Sh150,000 halafu niende nikauze kilo moja Sh3,000 kwa sababu haina faida yoyote na sukari haipatikani kwa hiyo ukikutana nayo unanunua kwa bei yoyote ili mradi wateja wako wasiikose dukani,” amesema Edwin.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live