Mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameagiza msako kwa vijana wanaobaka wanawake kwenye visima vya maji.
Senyamule ametoa agizo hilo katika Kata ya Chandama ambapo amesema lazima Polisi waweke kambi hapo.
Kauli ya kiongozi huyo imekuja baada kuibuka kwa hoja ya wanawake kubakwa wanapowahi kwenda kuchota maji umbali mrefu.
Kwenye Mkutano huo, hoja ya ubakaji iliteka mjadala ambapo viongozi wa eneo hilo walikiri kuwepo kwa matukio mengi yanayojirudia na hasa kwa wanawake wanaowahi alfajiri kwenda kutafuta maji.
Baadhi ya wanawake waliozungumza kwenye mkutano huo walieleza madhira hayo kwamba huwapata wakati wanakwenda kusaka maji.
Fatuma Maulid alisema maisha yao yamekuwa shakani kwa miezi ya kuanzia Juni hadi Desemba mvua zinapoanza kunyesha kwani kila mwanamke anakuwa kwenye hatari.
Fatma alisema ndoa nyingi zimevunjika katika Kata hiyo ambayo inaundwa na vijiji sita lakini mabinti wengi wanapata mimba na kukatiza masomo.
"Wanawake hatuna amani, hatuna wa kutusaidia kama si kupata maji kwa 'Walonjoro' (rika balehe) wanatusumbua kwani wanachimba visima kwa ajili ya kututega tu sasa ukikubali unapa maji ukikataa unabakwa na maji hupati," amesema Fatuma.
Kauli hiyo imemkera Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo na kuagiza viongozi kuanzia ngazi ya vijiji washughulike na watu hao ili wawe kwenye mikono ya sheria.
Chongolo amesema wabakaji lazima watakuwa wanajulikana lakini cha ajabu hakuna aliyekamatwa na kuwekwa ndani ikibidi kuhukumiwa ili iwe fundisho jambo alilosema huenda ulegevu unatokana na viongozi wa ngazi ya chini.