Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Chalamila awahimiza Watanzania kuliombea Taifa

Chalamila: Changamkieni Fursa Mkutano Wakuu Wa Nchi Afrika RC Chalamila awahimiza Watanzania kuliombea Taifa

Mon, 11 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka Watanzania kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani, upendo na umoja na wananchi wote pamoja na viongozi waishi na kufanya kazi kwa haki.

Chalamila amebainisha hayo jijini Dar e Salaam wakati akishiriki mkutano ulioandaliwa na Kanisa Halisi la Mungu Baba ukioongozwa na mada iliyosema: “Tanzania ni chanzo cha baraka kwa mataifa mengine.”

Amesema waumini wana wajibu wa kuliweka Taifa hili mikononi mwa Mungu kwa kuwa wana nafasi kubwa ya kulitegemeza Taifa lao kupitia maombi yao na amani ya Taifa iko mikononi mwao.

“Mna wajibu mkubwa wa kuliweka mikononi mwa Mungu Taifa hili. Mapambano na mabishano tuyaonayo tutapona kama tutaliweka mbele jina la Mungu baba mwenyewe,” amesema Chalamila.

Amesema siku hizi unapozungumzia amani, unazungumzia upatikanaji wa chakula ambao unapeleka usalama wa chakula. Aliongeza kwamba hiyo ndiyo sababu ya mataifa mbalimbali yalikutana hapa Tanzania kwa ajili ya kujadili masuala ya chakula.

Mkuu huyo wa mkoa amesema mafundisho ya kuzalisha kwa haki yanayotolewa na kanisa hilo yaende sambamba na kuwaombea viongozi wa Serikali ili nao wapate vipato vya haki kama watu wengine wanaozalisha kwa haki.

“Kuzalisha kwa haki siyo tu katika kanisa hili, ni pamoja na kuwaombea viongozi wa aina yangu na wa serikali hii, vipato vyao vizalishwe kwa haki. Vipato vya viongozi wa Serikali vikizalishwa kwa haki, Taifa limepona,” alisema mkuu huyo wa mkoa.

Chalamila amewataka Watanzania wasiwe watu wa kulalamika kwenye kila changamoto wanayokutana nayo, bali wawe sehemu ya kutoa majawabu kwa yote wanayokutana nayo mbele yao, iwe ni mazuri au mabaya.

Kwa upande wake, kiongozi wa kanisa hilo, Baba Halisi amewataka waumini wake kuishi kwa kuzingatia upendo na siyo imani zao kwa sababu zinawagawa lakini upendo unawaunganisha watu.

“Imani inatugawa lakini upendo unatuunganisha, kwa hiyo tunapoyatafakari haya, tuyatafakari kwa upendo. Amani, upendo na kuzalisha kwa haki ndiyo bustani halisi ambayo tunatakiwa kuishi wakati wote,” amesema Halisi.

Amesisitiza kwamba Tanzania ni chanzo cha baraka kwa mataifa mengine, hivyo Taifa likiwa chanzo cha baraka hakuna kulaumu. Alisisitiza kwamba hata ukiwa na nguvu kiasi gani, kama watu wako wanakulaumu, utashusha mikono chini kama Mussa alivyofanya wakati wa vita.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live