Mkuu wa Mkoa wa Kagera (RC), Albert Chalamila ameahidi kutekeleza kauli ya Serikali ya kuinua uchumi wa mkoa huo kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wa Kagera.
Ameyasema hayo jana Alhamisi Agosti 4, 2022 wakati akikabidhiwa ofisi na mtangulizi wake Meja Jenerali Charles Mbuge.
Chalamila ni miongoni mwa wakuu wa mikoa walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuapishwa Agosti 1, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mara baada ya kukabidhiwa, Chalamila amesema, kauli ya kuinua mkoa wa Kagera kiuchumi ilitolewa na Rais Samia alipotembelea mkoani humo mwaka huu.
Amesema yeye kama mkuu wa mkoa anaendelea kuisimamia kauli hiyo ili aweze kuinua uchumi wa mkoa huo na kuwaletea maendeleo wananchi.
"Nitalipitia kablasha la mkoa ili nijue niko wapi, natoka wapi na nakwenda wapi,” amesema na kuongeza:
“Baada ya hapo nitaweza kueleza ni wapi nianzie ila ile kauli ya Rais aliyoitoa wakati akiwa mkoani hapa ya kuinua uchumi nitaanza nayo katika kuifanyia kazi naomba wanakagera waniunge mkono."
Kwa upande wake, Meja Jenerali Charles Mbuge, amekabidhi majukumu matatu ya Kitaifa kwa Chalamila ili aweze kuyasimamia na kiyafanyia ikiwa ni pamoja na sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022, Kilele cha mbio za mwenge kitaifa Oktoba 14, 2022 pamoja na mradi wa bomba la mafuta.
Meja Jenerali Mbuge amemtaka pia mkuu huyo wa mkoa kuendelea kusimamia zao la kahawa na kuthibiti magendo ya zao hilo ili kahawa ilete tija kwa wakulima wa mkoa huo.
Naye katibu tawala wa mkoa wa Kagera, Toba Nguvila ameahidi kutoa ushirikiano kwa mkuu wa mkoa wa Kagera katika kuinua uchumi wa mkoa huo ili kuleta maendeleo ya Wanakagera na Taifa kwa ujumla.