Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amawataka Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) maarufu kwa jina la Mwendokasi, kuangalia namna ya kuongezeka muda wa kufanya kazi hadi kufikia saa 24 badala ya muda uliopo sasa.
Mbali na hilo pia amesema hafurahishwi na malalamiko yaliyokuwapo kwa muda mrefu juu ya kuchelewa kwa mabasi hayo jambo ambalo linawafanya wananchi kusubiri kituoni kwa zaidi ya saa 1.
Ametoa kauli hiyo leo Juni 27 wakati akizindua safari za mabasi hayo kati ya Gerezani hadi Mbagala rangi tatu ambayo imelenga kurahisisha huduma ya usafiri kwa watu wanaotaka kutembelea maonyesho ya sabasaba yanayotarajia kuanza kesho Julai 28, 2023.
Chalamila ameitaka Dart kuanza kuangalia namna ya kuongeza muda wao wa kazi ili kuhudumia watu wengi zaidi.
"Leo anzeni kuliangalia hili. Jambo ambalo sifurahishwi ni Dart kufanya kazi kwa saa kadhaa, nataka ikiwezekana wafanye kazi kwa saa 24 kama mtu ametoka saa saba akute basi kama saa 10 usiku akute basi,” amesema.
Amesema maana ya mwendokasi haimaaanishi kufanya kazi saa 1 asubuhi hadi saa 4 usiku na kwenda kulala.
"Watu wana wagonjwa wanashindwa kupanda magari kukiwa kuna mwendokasi watapanda kwenda hospitali," amesema.
Amesema mabasi yaliyosajiliwa ni mengi, huku akieleza kuwa anaamini idadi ya madereva ni mara mbili ya mabasi yaliyopo hivyo kufanya uwezekano wa kufanya kazi saa 24 kwa kupishana.
Akizungumzia wananchi kusubiri muda mrefu katika vituo amesema, atafanya ziara siku ya Jumamosi ya Julai Mosi, 2023 ili kusikiliza maoni ya Wananchi akishirikiana na Dart na yale yanayohitaji kurekebishwe yafanyiwe kazi
“Azma ya Rais (Samia Suluhu Hassan) ni kubwa ameweka fedha nyingi katika mradi huu, tuone maana halisi ya kuwa na basi liendalo kasi.
“Watanzania kusubiri saa 1 hadi 2 katika vituo hakuna maana ya kuwepo kwa basi hili, ni bora wangepanda basi la kawaida ili achelewe kufika kuliko kusubiri basi hili kwa muda wote huo, hivyo Jumamosi tutapita kusikiliza maoni yao,” amesema.
Amesema katika ziara hiyo anatarajia kufanya safari zake kati ya Gerezani na Mbezi.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), Deusdecity Casmir amesema mabasi 30 yametengwa kwa ajili ya safari ya Gerezani na Mbagala hadi maonyesho hayo yanapofikia tamati na kwa kuanzia magari 20 ndiyo yataanza kazi.
“Pia katika kurahisisha huduma ya usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam wanaotaka kutembelea maonyesho haya, tumeongeza vituo vitatu vya Sabasaba maonyesho, Mission (Kijichi) na Zakhem kabla ya kufika Mbagala Rangitatu,” amesema Casmir.