Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Aagiza Kupewa Orodha ya Walioacha Shule Sababu ya Bangi

B94d7ef3d4a6231ec11a072933e94705.jpeg RC Aagiza Kupewa Orodha ya Walioacha Shule Sababu ya Bangi

Wed, 1 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka amemwagiza Katibu Tawala (DAS) wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, Andrew Ng'hwani kuandaa orodha ya wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari walioacha masomo kwa sababu mbalimbali zikiwamo za kuvuta bangi na kumkabidhi ili kuchukua hatua.

Mtaka alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yaliyofanyika kitaifa katika Kijiji cha Pahi, Kata ya Pahi wilayani Kondoa mkoani Dodoma.

Ilikuwa ni baada ya Diwani wa Kata ya Pahi, Yakubu Kidula kulalamika kwamba baadhi ya wanafunzi katika shule za msingi na sekondari katika kata hiyo, wameacha shule kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kuvuta bangi.

Diwani Kudula alilalamika kwamba pamoja na juhudi za viongozi wa serikali ya kata kutaka kuwarudisha shuleni, imekuwa vigumu kutokana na wazazi wao kutotoa ushirikiano kwa viongozi hao.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Pahi, Amani Selle alikiri kuwepo kwa changamoto ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika eneo hilo kuacha masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ya kuvuta bangi, lakini juhudi za kuwarejesha shuleni bado zinaendelea.

Mtaka baada ya kusikiliza malalamiko hayo, alimtaka DAS kufuatilia katika shule za msingi na sekondari na kukusanya takwimu za idadi ya wanafunzi katika kila darasa na kila kidato walioacha masomo na sababu zilizosababisha ikiwemo hiyo ya kujiingiza katika vitendo vya kuvuta bangi.

"DAS, nisaidie kupata taarifa ya wanafunzi waliokatisha masomo ni wangapi kila darasa na kila kidato katika shule za msingi na za sekondari katika eneo hili," alisema.

Mtaka alisema kama wanafunzi hao wameshindwa kufunzwa na wazazi wao basi watafunzwa na ulimwengu na yeye ndiye ulimwengu mwenyewe, atawafundisha.

Mkuu wa mkoa huo pia aliwahimiza wananchi wa wilaya hiyo kusomesha watoto wao, ili kuwa na wasomi wengi kama Dk Ashatu Kijaji ambaye ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini.

Aliwaagiza wazazi wenye watoto katika shule za msingi na sekondari kwenda shuleni wakati wa kufunga shule wiki ijayo, ili kusikiliza matokeo ya watoto wao na kujua kama walikuwa wakisoma au walikuwa watoro.

Pia aliwaagiza wazazi watakaokuwa na watoto katika madarasa ya mitihani mwakani, yaani darasa la nne, la saba, kidato cha pili, nne na sita kuwapa wanafunzi hao nafasi ya kutosha kujiandaa kusoma na pia wawasaidie kujiandaa na kama wapo wawatumie vijana wanaosoma vyuoni kuwafundisha.

Mtaka alisema kati ya fedha Sh trilioni 1.3 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan nchini, Mkoa wa Dodoma umepata mgao wa Sh bilioni 14 kwa ajili ya kujenga madarasa, hivyo haipendezi wazazi kutopeleka watoto shuleni wakati shule zinajengwa.

"Si busara, wala haipendezi wakati madarasa yamejengwa, madawati yapo na walimu wamepelekwa shuleni, halafu watoto hawaendi shuleni," alisema.

Mtaka aliwahimiza wazazi kutumia fedha kidogo wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka na kubakiza kwa ajili ya kuwapa mahitaji watoto wao mwanzoni mwa mwaka yakiwemo madaftari, vitabu na sare za shule.

Aliwataka wananchi kutumia vizuri mvua chache za mwaka huu kwa kulima mazao kama mtama na alizeti ambayo yanahitaji mvua chache ili kuwasaidia kupunguza utapiamlo, udumavu na ukondevu ambao umekithiri mkoani humo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kondoa Mji, Mohamed Kiberenge alisema amepokea maagizo ya Mkuu wa Mkoa Mtaka ya kutoa agizo la kukusanya orodha ya watoto walioacha shule kwa sababu mbalimbali na wao watatekeleza.

Chanzo: www.habarileo.co.tz