Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RAS Songwe: Tumepigwa, mkurugenzi nakupa siku 21

Songwe WA0019 RAS Songwe: Tumepigwa, mkurugenzi nakupa siku 21

Thu, 7 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu tawala mkoani Songwe, Happines Seneda ametoa siku 21 kwa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ileje, Nuru Kindamba kumpatia majina ya watuhumiwa wa wizi wa vifaa vya ujenzi wa zahanati za Mtima na Shinji.

Pia amemuagiza kumpa maelezo ya sababu za kushinwa kusimamia miradi ya zahanati hizo mbili zilizopo katika halmashauri hiyo. 

Seneda, ameyasema hayo leo Jumatano wakati akikagua zahanati hizo na kubaini mapungufu kwenye usimamizi ya miradi hiyo ikiwemo uwepo wa taarifa zenye mkanganyiko.

Akiwa kwenye zahanati ya Mtima ambayo Serikali ilitoa Sh 50 milioni huku wananchi wakichangia Sh 20 milioni za ujenzi wa boma na matundu mapya ya vyoo, alibaini upotevu wa marumarua boksi 41 pamoja na vifaa.

Aidha, amebaini kuwa afisa manunuzi hajawahi kufika kwenye mradi huo toka uanzishwe na alipoulizwa alishindwa kutoa majibu ya msingi.

“Jengo limejengwa halina ramani, mkataba kati ya halmashauri na fundi haupo, vifaa havionekani, mkurugenzi hapa ulizembea hata ofisi ya manunuzi haijafika hapa, kuna kila dalili kuwa tumepigwa,’’ amesema Seneda.

Awali Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Dk. Zacharia Mollam amesema taarifa kuhusu ujenzi huo, zimechukuliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Afisa mtendaji wa kijiji hicho, Aston Mwaila amesema wagonjwa wanatembea kilometa 13 kufuata huduma za matibabu katika zahanati ya kata ya Mbebe hali inayosababisha wajawazito kujifungulia njiani.

Katibu tawala huyo pia ametembelea zahanati ya Shinji iliyojengwa kuanzia mwaka 2021 na kubaini kiasi cha Sh  32.5 milioni kilichotumika kujenga vyoo, mnara wa tenki la maji na chumba cha mama na mtoto na kubaini kasoro katika taarifa za ujenzi huo.

Kutokana na hali hiyo, Katibu Tawala huyo amemuagiza mkurugenzi huyo wa halmashauri kufanya uchunguzi ili walioiba vifaa vya ujenzi wa zahanati hiyo pia ufanyike.

Mkurugenzi huyo ameeleza kupokea maagizo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live