Vyuo vinakataa maombi yake, kisa amepata daraja la tatu hivyo hana sifa ya kusoma elimu ya juu.
Ameona isiwe tabu. Maarifa yake ya masomo ya Kemia , Fizikia na Biolojia aliyosomea kidato cha tano na sita, ameamua kuyahamishia katika uhalisia maishani. Sasa ameamua kuwa mjasiriamali akishirikiana na mafundi kutoa huduma kwa watu mbalimbali.
Ni Queen Mtega (20) msichana anayeamini katika uthubutu. Amebuni tovuti yake ya FundiPopote, akilenga kutoa huduma za ufundi kwa wananchi na kuondoa dhana ya watu kuwaona mafundi kama watu wasio na thamani.
Wazo la FundiPopote
“Sikuwahi kuwaza kuwa nitajikita katika masuala ya ufundi kwani awali niliwaza kujikita katika mazingira, lakini nilishindwa kutokana na changamoto mbalimbali,”anasema.
Baada ya kumaliza kidato cha sita Queen alichaguliwa kwenda kushiriki mafunzo ya jeshi, lakini baada ya kurejea kutoka jeshini siku moja alikwenda kumtembelea rafiki yake. Aliomba maji ya baridi, akaletewa ya moto. Mama wa rafiki yake alimweleza kuwa jokofu la kuhifadhia maji limeharibika.
“Ikabidi nimuulize mama yake kwa nini lisitengenezwe? Mbona linaweza kutengenezeka? Akasema mafundi wenyewe hamna au unaweza ukampa akatapeli tu kwa hiyo bora nitafute fedha ninunue nyingine; hapo ndipo wazo la FundiPopote likanijia,”anasimulia.
Anasema huo ndiyo mwanzo wa wazo la FundiPopote na kugundua kuwa vitu vingi vya vinaharibika kwa kukosa ufumbuzi.
‘’Watu wanajua kuwa kitu kikiharibika ndio basi tena hakiwezi kutengenezeka tena, kwa hiyo dhana hii inasababisha vitu kutupwa vikiwa bado vinaweza kufanya kazi,”anaeleza na kuongeza:
“Kwa hiyo nilianza kutengeneza tovuti hii kama jukwaa la mafundi mbalimbali na kupeana hamasa jinsi ya kutengeneza uaminifu kwa wateja wao,” anaongeza.
Baaadaye anasema alianza kuzunguka katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutafuta mafundi ambapo hadi sasa amefanikiwa kupata mafundi 60 kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.
Anachokifanya anasema ni kuandika taarifa za mafunzo ikiwamo maeneo wanapopatikana, picha zao, aina ya ufundi wa mtu, mawasiliano na taarifa nyingine.
“Kwa hiyo mteja akiingia kwenye tovuti ya Fundipopote atakuta taarifa kamili ya mafundi hao, lakini cha msingi ni kwamba fundi yeyote lazima awe na kibali kutoka kwa uongozi wa mtaa ili kuzuia utapeli utakaojitokeza,” anaongeza.
Kuhusu malipo anasema ili kazi ifanike vizuri bila kuwapo kwa utapeli anatarajia kuanzisha mfumo wa malipo ambapo malipo yote yatapitia kwenye tovuti ya Fundipopote
Mafanikio yake na changamoto
Imezoeleka kwa wengi kuwa mafaniko ni pale mtu anaposema aina na ukubwa wa mali anazomiliki kama magari na nyumba, lakini kwa Queen anajivunia kutimiza ndoto yake ya kuwa mjasiriamali wa kidijitali.
“Najivunia ni kwamba ndoto zangu za kuwa mjasiriamali zinatimia, yaani naona kabisa naanza kufikia malengo yangu niliyojiwekea tangu nikiwa shule,”anasema.
Kupitia mradi wake wa Fundipopote, ameweza kupata mialiko ya semina mbalimbali ya jinsi ya kuongeza ufanisi katika kazi zake ambapo anajivunia kujuana na watu mbalimbali.
Kama ilivyo usemi kuwa ua zuri halikosi miba, Queen anapitia changamoto mbalimbali hasa za kuwatafuta mafundi, kwani wengi wanaonyesha hali ya kutomwamini.
“Lakini pia ili kufika katika maeneo mbalimbali inabidi nitumie usafiri wa daladala au hata kutembea wakati mwingine. Kwa hiyo unakuta muda mwingi naumaliza barabarani, lakini mimi sikati tamaa kwa huwa huo ndiyo ujasiriamali,”anasema.
malengo yake siyo tu kuendesha mradi wake kwa njia ya mtandao bali kuwa na kampuni kubwa itakayotambulika na kuwa na mafundi zaidi ya 100 itakayohudumia wateja katika maeneo mbalimbali.
Anaongeza kuwa lengo lake ni kuondoa pengo la uaminifu kati ya mteja na mafundi, kwa sababu kwa mafundi wasio waaminifu hawawezi kuendelea kimaisha.
“Kwa hiyo nataka kujenga uaminifu na kuufanya ufundi kuwa na thamani lakini pia kuondoa ile dhana ya kuuona ufundi kama kazi isiyo na hadhi. Unakuta hata fundi mwenyewe anafanya kazi kwa kutojiamini, hivyo kujikuta akiishia kutengeneza vitu vya nyumbani kwake,”anasema.
“Ndoto yangu ni kuona kwamba vitu haviharibiki na kutupwa ovyo; hii inarudisha maendeleo nyuma. Unakuta mtu kwa mwaka ananunua vitu zaidi ya mara tatu kwa sababu vinapoharibika havitengenezwi vunatupwa tu,”.
Hata hivyo, anasema kupitia Fundipopote badala ya kutupa sasa vitakwenda kutengenezwa kwa hiyo hasara ya kutupa vitu pindi vinapoharibika na na kununua vingine itakuwa historia.
“Lakini pia nina ndoto ya kuwa mhamasishaji, kwani kuna tatizo kwa vijana Tanzania kuogopa kuthubutu. Mtu anaweza akafikiria kitu lakini akawa mvivu wa kutekeleza,”anasema na kuongeza kuwa:
“Kwa hiyo nataka nihamasishe vijana wenzangu kwamba bila kujali elimu yako, bila kujali umri unaweza ukafanya makubwa katika jamii yetu mimi pamoja na kusoma masomo ya sayasi lakini ndoto yangu haikuwa kuwa daktari wala kuajiriwa bali kujiajiri mwenyewe,”.