Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pwani yaeleza siri ya kuwa na viwanda vingi

5840ad8b9bd3a7b3b94d92311e01cd37 Pwani yaeleza siri ya kuwa na viwanda vingi

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKOA wa Pwani umefichua siri ya kuwa na viwanda vingi kuwa ni kutokana na viongozi kuzungumza lugha moja kuanzia ngazi ya kitongoji, kuondoa urasimu kwa wawekezaji na kutowavumilia maofisa wenye urasimu.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha jana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo wakati wa ufunguzi wa Kongano la Viwanda linalohusisha shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika eneo moja dogo au kubwa zikihusisha kuendeleza bidhaa kwa kuhusisha wadau wengine wa maendeleo wanaonufaika na mnyororo wa thamani wa bidhaa husika.

“Kikubwa kilichofanikisha hilo ni kuondoa urasimu ambao umeonekana kuwa ni changamoto kubwa kwa baadhi ya maeneo na kukatisha tamaa wawekezaji kutokana na kuzungushwa wanapotaka kuwekeza ndani ya mkoa wa Pwani,” alisema.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kongamano hilo ni mkusanyiko wa viwanda vilivyo karibu vinavyofanya shughuli zinazofanana au kushabihiana vikisaidiwa na watoa huduma mbalimbali.

"Mkoa ulijipambanua tangu mwaka 2015 kuwa ukanda wa viwanda ambapo kwa mwaka huo tulikuwa na viwanda 395 na hadi mwaka jana tumefikia viwanda 1,236, vikubwa vikiwa 68, vya kati 112, vidogo na vidogo kabisa 888, hivyo kuendelea kuunga mkono nchi kuwa ya viwanda chini ya uongozi wa Rais John Magufuli.”

“Kongano hili ni njia ya kutambua faida za kiushindani kwa kuwezesha na kuimarisha uunganishwaji na ushirikiano baina ya wadau mbalimbali waliopo kwenye mnyororo wa thamani na unawezesha wajasiriamali kupata fursa na faida nyingi kama vile kupata teknolojia, kuongeza ujuzi, kupata taarifa, masoko na huduma wezeshi kama vile TBS.”

"Mkoa utaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa dhana ya viwanda kwa kuanzisha viwanda vidogo ili kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano awamu ya pili 2016-2017 na 2020-2021unazozitaka halmashauri kuendeleza kongano na kazi zinazolenga kuimarisha upatikanaji wa malighafi za viwanda vya ndani," alisema Ndikilo.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Teknolojia na Uendelezaji Viwanda (Sido), Emanuel Saiguran alisema dhana hiyo ilianza mwaka 2006 kutoka Sweden ukiwa ni mradi wa miaka mitano unaofadhiliwa na Sweden na imekuwa na manufaa makubwa na kuzalisha ajira nyingi.

Alisema dhana hiyo imeleta mafanikio kwenye mikoa minane ya Morogoro, Dodoma, Singida, Shinyanga, Mwanza, Kilimanjaro, Manyara na Kagera ambapo wanaendelea kuwajengea uelewa kutambua rasilimali zinazowazunguka ili ziwaongezee kipato.

Naye Meneja wa Sido mkoa wa Pwani, Beata Minga alisema wamejipanga kuweka mikakati ya kuanzisha kongano kwenye mkoa huo ambao bado haujaanzisha dhana hiyo ili kutumia fursa hiyo kuibua viwanda na kuwa na sauti ya pamoja.

Chanzo: habarileo.co.tz