Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Profesa Mkenda alipia kodi waliounguliwa nyumba Rombo

Mkenda Niaba Mkuu wa wilaya ya Rombo Kanali Hamis Maiga akikabidhi baadhi ya vitu kwa niaba

Fri, 10 Feb 2023 Chanzo: Mwananchi

Wananchi 32 kutoka kaya 7 zilizokumbwa na ajali ya moto na kuachwa bila makazi katika Kijiji cha Mbomai, kata ya Tarakea Motamburu, wilayani hapa wamelipiwa kodi ya miezi miwili na Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda.

Pamoja na kuwalipia kodi ya pango, amewapa msaada wa vitanda, magodoro, vyakula pamoja na vifaa mbalimbali vya majumbani.

Ajali hiyo ya moto ilitokea usiku wa Februari 6, 2023 na kuteketeza vyumba 11 vya wapangaji na kuunguza mali zilizokuwemo ndani kama vyakula, mavazi na fedha ambapo wananchi hao hawakuweza kuopoa chochote.

Akikabidhi misaada hiyo leo Februari 10, kwa niaba ya mbunge huyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Kanali Hamis Maiga amemshukuru kwa kujitoa kwa wananchi wake.

"Baada ya tukio hili la moto kutokea Serikali tulikuwa bega kwa bega kuwasadia wananchi hawa, lakini leo tunamshukuru Mbunge wetu, Profesa Mkenda kwa kutoa msaada huu mkubwa kwa wananchi hawa.

"Leo tumewapatia vyumba vya kuishi wananchi hawa kwa muda wa miezi miwili ili wasiendelee kuhangaika kuomba hifadhi kwa watu,"amesema Kanali Maiga.

Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa misaada hiyo, wananchi hao wamemshukuru mbunge huyo, kwa namna alivyowakimbilia kwa kuwapatia hifadhi ya makazi na vyakula.

Lidya Mkwizu, mmoja wa waathirika hao wa moto amemshukuru mbunge huyo kwa kuwapa hifadhi ya makazi na vyakula na kusema tangu wapatiwe na janga hilo amekuwa nao bega kwa bei kuhakikisha wanakula na kupata hifadhi ya makazi.

"Tunaishukuru Serikali yetu, tangu tupate matatizo hawajatuacha, walishirikiana na sisi wakahakikisha tunakula na kuvaa na watoto wakaenda shule na tunamshukuru mbunge wetu kwa kutuletea vyakula, kutupa hifadhi ya makazi na kutulipia miezi miwili ya pango, Mungu ambariki sana," amesema.

Kwa upande wake Restuta Mzava, mwathirika mwingine wa ajali hiyo ya moto, amesema upendo ambao umeonyeshwa na viongozi hao umewafuta machozi kwa kuwa wapo nao tangu wapatwe na janga hilo na kuhakikisha wanakuwa sehemu salama.

"Hali yetu ilikuwa ni mbaya sana baada ya kupata janga hili la moto, tunashukuru tumeletewa vitanda, magodoro, vyakula, sasa hivi tunaishi maisha mazuri," amesema.

Naye Halifan Amiri, amesema kwa misaada hiyo ambayo viongozi wameendelea kuwapatia wanajiona kama hawajapungukiwa na chochote kwa kuwa wamepata mahali pazuri pakulala na watoto wao wameweza kwenda shule baada ya kununuliwa sare za shule.

"Upendo ambao tumekuwa nao kwa viongozi wetu tumejiona kama hatujapungukiwa maana viongozi wetu hawa wametukimbilia na wamekuwa na sisi bega kwa bega, hakuna siku ambayo hatujaona viongozi wetu hapa, kwa kweli wametupigania sana," amesema.

Akizungumzia msaada huo, Katibu wa Mbunge wa Rombo, John Mrina amesema ofisi hiyo ya mbunge itaendelea kuwa bega kwa bega na wananchi hao na kuhakikisha wanarudi katika maisha yao ya kawaida.

Chanzo: Mwananchi