Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Profesa Mbarawa awaonya waharibifu wa vyanzo vya maji

28236 Pic+mbarawa TanzaniaWeb

Thu, 22 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi wanaofanya shughuli za uharibifu wa vyanzo vya maji kuacha na wanaokaidi wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Profesa Mbarawa ametoa kauli hiyo leo Jumatano Novemba 21, 2018 wakati akishiriki shughuli ya upandaji miti kwenye chanzo cha maji Mto Kizinga, Mbagala jijini Dar es Salaam.

Amesema ili kuwe na vyanzo endelevu vya maji nchini lazima vitunzwe na sheria ya kukaa mita 60 inapaswa kuzingatiwa na wale ambao wanakaidi wachukuliwe hatua.

"Ili tuwe na maji endelevu lazima tupande miti, halafu unaondoa shughuli mbalimbali kama za kilimo ambazo kwa sehemu kubwa ndio wanaosababisha vyanzo kukauka," amesema Profesa Mbarawa.

"Ulimaji holela si sahihi, baadhi ya watu wanalima na kutumia mbolea ambazo zinaharibu vyanzo vya maji, sitakubali lazima tuchukue hatua na Watanzania wapate maji lakini watoto na wajukuu wetu wakute maji," ameongeza.

Profesa Mbarawa ametoa wito kwa mamlaka za maji kuhakikisha wanapanda miti kwenye vyanzo vya maji ili kuvilinda visikauke kwani hali ilivyo sasa hairidhishi.

Waziri huyo ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wote wanodaiwa bili za maji kuhakikisha wanalipa kabla ya kukatiwa huduma hiyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva amesema chanzo hicho cha Kizinga kilichokuwa kinahudumia Jiji la Dar es Salaam kilianzishwa mwaka 1949.

"Lazima chanzo hiki tukitunze, wale wote wanaoendesha shughuli kando ya vyanzo vya maji, wanaacha na mimi niko tayari kusimamia sheria," amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Maji Bonde la Wami/Ruvu, Saimoni Ngonyani amesema watasimamia sheria kama inavyoelekeza ya utunzaji wa vyanzo vya maji.

Ngonyani amewataka watumiaji wote wa maji ya visima kulipa ada zao na wanaokaidi watapelekwa mahakamani kama walivyotangaza hivi karibuni kwa hoteli na kampuni 100 zilizoshindwa kutekeleza agizo hilo.

Katika hili,  Profesa Mbarawa ametoa wito kwa wananchi wanaoishi kando ya mtandao wa maji wa Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasa) kutotumia ya kisima na kuunganishiwa na ya Dawasa. Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja amesema kuna tatizo kubwa la vyanzo vya maji kwani vinaharibiwa.

Amesema wameanzisha kampeni ya kurejesha maji mitoni na Desemba 9, 2018 wanakwenda kupanda miti mingi katika mto Ruvu ambao umeharibiwa.

Kuhusu chanzo cha maji cha Mto Kizinga, amesema awali ulikuwa unazalisha lita milioni tisa lakini baada ya uharibifu zikashuka hadi milioni nne na sasa zimepanda hadi milioni saba.



Chanzo: mwananchi.co.tz