Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prof Mikidadi afariki dunia, azikwa Morogoro

Prof Mikidadi Afariki Dunia.jpeg Prof Mikidadi afariki dunia, azikwa Morogoro

Mon, 5 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanazuoni maarufu, Profesa Juma Mikidadi amefariki dunia jana katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mkoani Morogoro alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu kwa muda wa mwezi mmoja.

Dk Abdallah Tego aliyewahi kufanya kazi na Profesa Mikidadi katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUM), ameliambia Mwananchi leo Jumatatu Desemba 5,2022 kwamba msomi huyo alifariki dunia jana saa usiku katika hospitali hiyo.

“Nimezungumza na moja wa kijana wake, amenieleza taarifa hizi na tayari ameshazikwa leo saa nne asubuhi katika makaburi ya Mkundi Morogoro,” amesema Dk Tego ambaye ni mhadhiri wa Mum.

Profesa Mikidadi aliyezaliwa Julai 7 mwaka 1949 wilayani Kibiti mkoani Pwani ni miongoni mwa wasomi wa falsafa ya sheria na sharia nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.

Amewahi kufundisha Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya kuanzia mwaka 1991 hadi 1994 na mwaka 1995 aligombea ubunge wa Kibiti katika uchaguzi mkuu wa vyama vingi na kushinda, alifanikiwa kudumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 2005 kisha kurejea kufundisha chuo.

Mwaka 2006 Profesa Mikidadi alianza kufundisha katika akiwa mkuu wa kitivo cha sheria na sharia.

Akizungumzia Profesa Mikidadi, Dk Tego amesema enzi za uhai wake msomi huyo alifanikiwa kuwafundisha na kuwajengea uwezo vijana wengi.

“Alifanikiwa kuwasaidia vijana waliokuwa wakifanya tafiti zao mbalimbali za falsafa ya dini ya Kiislamu, ametoa mchango mkubwa kwa menejimenti ya Mum ya namna ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“Wiki iliyopita nilitaka kwenda hospitali kumjulia, hali lakini sikufanikiwa baada kupata dharura ya kuja Dar es Salaam na jana nikapata taarifa za msiba wake,” amesema Dk Tego.

Katibu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema Profesa Mikidadi ni mmoja ya wanazuoni aliyekuwa na mchango katika dini na shughuli za kijamii kupitia siasa.

“Nimemfahamu kwa muda mrefu, ameweza kufanya mihadhara katika majukwaa mbalimbali ya Kiislamu, alikuwa kiongozi mwenye mchango kwa jamii na dini, ndivyo viongozi wanavyotakiwa,” amesema Sheikh Ponda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live