Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Povu jeupe lazua taharuki Morogoro

Povu Balaaaaa.jpeg Povu jeupe lazua taharuki Morogoro

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Morogoro. Idara ya Afya Manispaa ya Morogoro imewaonya wananchi wa Kata za Tubuyu na Tungi kuacha kutumia maji ya Mto Ngerengere baada ya maji hayo kutoa mapovu yaliyozua taharuki.

Baadhi ya wananchi wamekuwa wakisema mapovu hayo ni mawingu yaliyoanguka kutoka angani mkoani Morogoro.

Kupitia video fupi iliyosambaa mitandaoni wananchi walisikika wakidai mapovu hayo ni mawingu yamenguka kutoka angani, lakini mamlaka mkoani Morogoro zimekanusha hili zikisema yametokana na kemikali zilizomwagika kutoka kwenye lori.

Akizungumza na gazeti hili mjini hapa jana, Ofisa Afya Manispaa ya Morogoro, Ndimile Kilatu alisema maofisa wa idara hiyo walifika eneo la Tubuyu B saa mbili asubuhi juzi kufuatilia chanzo cha mapovu katika korongo linalopitisha maji wakati wa mvua na kuyapeleka Mto Ngerengere na kubaini ni malighafi ya kutengenezea sababu, iliyomwagika Januari 17, mwaka huu kwenye maegesho ya malori katika eneo la Nane Nane.

Kilatu alisema walitoa elimu na kuwazuia wananchi wa Tubuyu B wanaotumia maji ya mto huo na wengine, kutoyatumia mpaka idara hiyo na nyingine watakapopima kubaini nini chanzo cha mapovu hayo.

“Timu ya idara ya afya manispaa na wenzetu wa Mamlaka ya Bonde la Wami-Ruvu tulifuatilia chanzo cha mapovu na kubaini malighafi ya kutengenezea sabuni iliyomwagika kutoka kwenye lori lililokuwa limebeba madumu yenye malighafi hiyo litoka Dar es Salaam kwenda Zambia au DRC Congo,” alisema.

“Kati ya madumu hayo, mawili au matatu yalianguka na kupasuka na malighafi hiyo ikamwagika ardhini.,” alisema.

Kilatu alisema baadhi ya wananchi waliichota wakidhani ni bidhaa yenye thamani kwao, hivyo walienda nayo nyumbani.

Idara hiyo imewataka wote waliochukua malighafi hiyo waipeleke katika idara hiyo kwa ajili ya uchunguzi.

“Mvua iliyonyesha siku mbili hizi imesafisha mabaki ya kemilikali hiyo na kuipelekwa kwenye vyanzo vya maji katika Mto Ngerengere na kutokana na maporoko ya maji, imezalisha povu. Tunafanya uchunguzi wa kimaabara tutatoa majibu,” alisema Kilatu.

Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Mkoa wa Morogoro, Hidaya Senga alisema tukio hilo halihusiani na idara hiyo, licha ya kuwa wananchi wamewapa taarifa juu ya kuonekana kwa mapovu hayo.

“Si tukio linalohusu mamlaka ya hali ya hewa ila watalaamu wetu wa idara wamefika eneo la tukio, mimi nikiwemo. Inaonyesha lile povu kuna kemikali imemwagika sehemu na ilipoingia kwenye maji hasa eneo lenye maporomoko imezalisha povu jeupe,” alisema Hidaya.

Alisema wananchi waliowapigia simu walifikiri ni barafu, lakini walipofika eneo la tukio waliona povu limezalishwa na maji yaliyokuwa yakitiririka kwa kasi na kuzalisha povu, ambalo wananchi wamelitafsiri kuwa mawingu yameanguka.

Meneja huyo amelisema hakuna mawingu yanayoweza kuanguka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live