Mkurugenzi ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Shabani Juma amelishukuru Shirika la Posta Tanzania kwa kuwaletea mifuko 300 ya saruji kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Juma ameyasema hayo leo Julai 8 baada ya kupokea mifuko hiyo, akisema imefika kwa wakati kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya huduma za jamii.
"Tulipeleka maombi taasisi nyingi za Serikali na binafsi kuomba tupatiwe vifaa mbalimbali vya ujenzi kwa ajili ya Shule, vituo vya afya, kituo cha polisi na miradi mingine mbalimbali ila tunalishikuru Shirika la Posta kwa kuwa wa kwanza kuitikia maombi yetu na kutupa msaada wa Saruji," ameeleza Shaban Juma.
Katika saruji hiyo, mifuko 150 imepelekwa kwenye shule za vijiji vya Ngomalusambo, Majalila (Mpanda Ndogo) na Katobo (Silonge) kwa ajili ya ujenzi wa sakafu za madarasa.
Pia mifuko 100 imepelekwa katika vijiji vya Mgansa na Isubangala kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati, pamoja na mifuko 50 kwa ajili ya jengo la kituo cha Polisi la Mpanda Ndogo.
Tukio hilo limeshuhudiwa na Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso aliyeeleza kufurahishwa kwake na namna Shirika hilo lilivyo karibu na jamii kupitia huduma zake kwa jamii huku akivitaka vijiji vilivyopokea saruji hiyo vikaitumie vizuri.
Akikabidhi mifuko hiyo kwa niaba ya Postamasta Mkuu, Mkurugenzi wa Shughuli za Posta, Arubee Ngaruka, amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, Selemani Kakoso kwa kuwa mstari wa mbele kulitangaza shirika hilo kwenye mageuzi makubwa yaliyofanyika katika kipindi kifupi.
Amesema mbali na shirika hilo kusaidia jamii katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii, limeweza kukua kimapato na kiuchumi siku hadi siku hivyo utoaji wa mifuko hiyo ya saruji ni sehemu ya shirika kurudisha fadhila kwa jamii inayolizunguka.
Aidha Arubee ametumia fursa hiyo kuwaeleza Wananchi wa Wilaya ya Tanganyika huduma zinazotolewa na shirika hilo ikiwemo Usafirishaji wa haraka kupitia EMS, usafirishaji wa kawaida wa Posta, usafirishaji wa mizigo mikubwa.