POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam imeua majambazi wawili wakati wa majibizano ya risasi usiku wa kuamkia Jumatano.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Mrakibu Msaidizi wa Polisi Muliro Muliro amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kamanda Muliro amesema watu hao walipoteza maisha kutokana na majeraha ya risasi wakati wakijaribu kuwashambulia polisi eneo la Tabata Liwiti baada ya kuwa wametiliwa shaka.
“Kulikuwa na watuhumiwa watatu kwenye pikipiki na walipobaini walikuwa wakifuatiliwa walianza kuwafyatulia risasi polisi ambao nao walijibu,” amesema.
Watuhumiwa hao wakiwa kwenye mwendo kasi waliyumba, kuanguka na wawili walianza kukimbia kwa miguu huku wakipiga risasi hovyo.
Kamanda Muliro amesema baada ya hali hiyo ndipo polisi walipowashambulia na kuwajeruhi vibaya sehemu mbalimbali za miili yao ambapo mmoja wao alifanikiwa kukimbia na pikipiki.
Amesema baada ya kupekuliwa mtuhumiwa mmoja amekuwa akiwa na silaha aina ya Browing yenye namba za usajili 75C51374 TZCAR NO 105413 ikiwa na risasi nne ndani ya kasha.
Kamanda huyo wa polisi amesema uchunguzi wa awali umebainika mtuhumiwa aliyekutwa na silaha Saidi Mgongwe (56) aliwahi kufungwa jela miaka 30 mwaka 1995 kwa tuhuma za unyang’anyi wa kutuhumia silaha na kutoka gerezani 2015.
Amesema pia uchunguzi mwingine umebaini watuhumiwa wa ujambazi waliofariki walihusika katika unyanga’anyi kwa kutumia silaha Agosti 21,2020 usiku katika kijiji Mpokozi-Mwandege, Vikindu Mkoa wa Pwani.
Katika tukio hilo watuhumiwa hao walimjeruhi Mussa Hassani Mazwazwa na kupora shilingi laki saba, seti ya telesheni na simu ya mkononi pamoja na silaha iliyokamatwa eneo la Tabata na kwamba majeruhi anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na ya CCBRT.