Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi yanasa mabasi 6 misiba feki

1ac7de66bf578f1ccf1a29aa4fe5d888 Polisi yanasa mabasi 6 misiba feki

Thu, 24 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JESHI la Polisi mkoani Morogoro limekamata mabasi sita yakisafirisha abiria yakiwa na mashada ya maua kuashiria yanasafirisha majeneza yenye miili ya marehemu wakati ni uongo.

Mabasi hayo madogo yalikamtwa usiku wa kuamkia jana katika kizuizi cha polisi kiliyowekwa eneo la Kingolwira katika Manispaa ya Morogoro, Barabara Kuu ya Dar es Salaam – Morogoro.

Juni 21, mwaka huu saa nne usiku basi dogo lililotumia uongo kama huo liligongana na magari mengine mawili eneo Nane Nane katika manispaa hiyo na kusababisha vifo vya watu tisa.

Ajali hiyo ilihusisha basi hilo aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili T 689 DUK likitoka Dar es Salaam kwenda Mbeya likagonga kwa nyuma gari aina ya Toyota Cresta lenye namba za usajili T563 ASA na baadaye Coaster likagongana uso kwa uso na lori lenye namba za usajili T658 DJZ mali ya Kampuni ya Dangote.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Fortunatus Musilimu alisema kati ya mabasi hayo sita manne yalitoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na mawili yalitoka Kahama mkoani Shinyanga yakienda Dar es Salaam.

Kamanda Musilimu aliyasema hayo jana katika Kituo Kidogo cha Polisi cha Kingolwira alipokuwa akitoa taarifa kwa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Wilbroard Mutafungwa.

“Hayakuwa na majeneza wala kitu chochote ila waliweka mashada ya maua na yamezuiliwa na wahusika kuendelea kuhojiwa,” alisema Kamanda Musilimu.

Aliongeza, “Tunawahoji wanakwenda wapi na gari mojawapo lililokutwa na mashada ya maua na abiria wao walidai wanakwenda kwenye msiba…tumelizuia hakuna jeneza la mwili wa marehemu tunataka kudhibiti huu ujanja ujanja waambieni wale wanaotumia magari haya wafuate utaratibu na operesheni hii ni endelevu kwa madereva wote na hatua kali za kisheria zitachukuliwa wenye kubainika na makosa.”

Alisema mabasi mengine madogo sita yaliyokuwa na mashada ya maua yalikaguliwa na kukutwa na majeneza yenye miili na wahusuka waliruhusiwa kuendelea na safari.

Kamanda Mutafungwa alisema kuanzia sasa katika mikoa yote vizuizi vya ukaguzi barabarani vitaongezwa na kuimarishwa hasa usiku.

“Vipo vituo Dar es Salaam kwenda mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, pia vipo Mbeya, Tukuyu, Njombe na Songwe, Kilimanjaro eneo la Himo, Morogoro stendi ya Dodoma na Mikumi...sasa ninawalekeza wamiliki wa magari haya wafuate sheria zote na abiria hasa wafanyabiashara kuanzia leo wasipande haya magari ili kuepuka kusumbuliwa,” alisema Kamanda Mutafungwa.

Alimtaka mmiliki wa basi dogo lililosababisha ajali na vifo na dereva aliyekuwa akiliendesha wajisalimishe kituo cha Polisi ndani ya saa 24 kuanzia jana.

Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Morogoro, Andrew Mlacha alisema operesheni ya ukaguzi wa mabasi madogo katika wiki moja iliyopita magari zaidi ya 25 yenye makosa yalikamatwa na kulipishwa faini na kutakiwa kurekebisha makosa.

“Kwa sasa tumeongeza operesheni ili kudhibiti ajali, magari lazima yakaguliwe na kufungwa vidhibiti mwendo na iwapo inaharibika abiria anakuwa na haki zake za msingi, lakini kwa sasa magari haya hayatoi risiti, hayana kituo maalumu na hata bima zake ni za mashaka,” alisema Mlacha.

Chanzo: www.habarileo.co.tz