Siku 10 baada ya Linda Lugala kukutwa amekufa kwenye nyumba ya kulala wageni Kibaha mkoani Pwani, Jeshi la Polisi mkoani humo limesema linaendelea na msako ili kumpata mhusika wa tukio hilo.
Linda alifika kwenye nyumba hiyo Aprili 4, 2023 saa sita usiku akiwa ameambatana na mwanaume na walichukua chumba na kulala.
Siku iliyofuata kabla ya saa 12 alfajiri mwanaume aliyekuwa naye aliondoka na kumtaka mlinzi wa nyumba hiyo ya wageni kutomuamsha Linda mapema, akisisitiza kuwa anapaswa kupumzika kwa kuwa amechoka sana.
Mlinzi huyo, Banyonga Hamisi akizungumza na Mwananchi Digital amesema hakusikia kama wawili hao waligombana wakiwa chumbani, "walikuja wakiwa na furaha na walionekana ni watu wanaopendana sana. Wakachukua chumba na kufanya malipo wakaenda kulala."
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Piusi Lutumo jana Ijumaa Aprili 14, 2023 alizungumzia tukio hilo akisema walipokea taarifa ya tukio hilo na kufika eneo la tukio mapema.
"Sisi tunaendelea na msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa au watuhumiwa wa kosa la mauaji na taarifa tulipokea Aprili 4 mwaka huu kutoka kwa mmiliki wa nyumba hiyo ya kulala wageni hivyo maofisa wa Polisi walifika na kukuta hali hiyo," amesema
Amesema walichukua mwili wa marehemu na kuupeleka hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi na baada ya uchunguzi kufanyika ilibainika amefariki na walikabidhi mwili kwa ndugu na kusafirishwa kwenda mkoani Iringa kwa ajili ya mazishi.
Ametoa wito kwa wafanyabiashara hasa wa nyumba za kulala wageni kufunga kamera za usalama kwenye majengo yao Ili kuwabaini watu wanaofika kwa nia mbaya.
Katika maelezo yake Hamisi amesema mwanaume huyo alitoka asubuhi na kusema kuwa watakuwa katika nyumba hiyo ya kulala wageni kwa siku mbili na alilipia Sh15,000, lakini ilipofika saa 4 asubuhi wakati wa kufanya usafi waligundua Linda amefariki na kutoa taarifa polisi.