Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza linapenda kutoa taarifa ya tukio la watoto wawili mapacha waliokufa maji baada ya kutumbukia kwenye Lambo la maji yaliyokuwa yametuama mita chache kutoka kwenye nyumba yao wakati wanacheza.
Tarehe 23.04.2023 muda wa saa 14:00 mchana, huko katika kijiji cha Runele, Kata ya Hungumalwa, Tarafa ya Nyamilama Wilaya ya kwimba, kuliripotiwa taarifa ya watoto wawili ambao wazazi wao wanaitwa Jimuku Rozalia, miaka 28 na Avelina Nkwaya, Miaka 20, wote wakulima na wakazi wa kijiji cha Runele wa jinsia ya kiume ambao ni Kulwa Jimoku na Doto Jimoku, wote wakiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi sita, waliokufa maji wakati wanacheza nje kidogo ya nyumba yao ambapo walitumbukia kwenye lambo la maji lililopo Mita 30 kutoka kwenye nyumba yao ambalo limetengenezwa na wazazi wao kwa lengo la kuhifadhia maji ya kunyweshea mifugo yao.
Chanzo cha tukio hilo ni michezo ya watoto na uzembe wa wazazi kutokuwa makini kwa kuangalia watoto hao kwani wakati tukio linatokea wazazi wao walikuwa wanaendelea na shughuli za kilimo nyumbani hapo.
Miili ya Kulwa na Doto imefanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya wilaya ya Kwimba na kukabidhiwa kwa ndugu kwa mazishi.
Jeshi la Polisi Mkoa Wa Mwanza linaendelea kutoa wito kwa wazazi/walezi kutimiza jukumu lao la msingi la malezi kwa watoto na sio kuwaacha bila uangalizi wa mtu mzima hususani katika kipindi hiki cha mvua ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.