Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wanamsaka anayedaiwa kuwabaka watoto watano Arumeru

RPC MASEJO 660x400 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo

Mon, 3 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limeanza msako wa kumkamata mzee wa miaka 55 (jina linahifadhiwa) mkazi wa Kijiji cha Shangarai, Kata ya Ambureni kwa tuhuma za kuwabaka watoto watano kwa nyakati tofauti.

Taarifa ya mtu huyo ilitolewa hivi karibuni kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara aliyoifanya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda wakati akisikiliza kero za wananchi Halmashauri ya Meru.

Makonda ameliagiza Jeshi la Polisi kusaka na kumkamata mtu huyo ili achukuliwe hatua za kisheria.

Akizungumza na Mwananchi leo Jamatatu Juni 3, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema bado wanaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo.

"Tutawapa taarifa tukimpata, kwa sasa bado askari wetu wako kazini kushughulikia suala hilo,” amesema Masejo.

Awali, mmoja wa watoto wanaodaiwa kubakwa mwenye umri wa miaka minane akizungumza kwenye mkutano baada ya kunyoosha mkono na kupewa kipaza sauti, alijitambulisha lakini akashindwa kuzungumza akaishia kulia kwa sauti.

Hata hivyo, kwa kuwa aliongozana na bibi yake, ilibidi achukue kipaza sauti na kuanza kusimulia mkasa mzima.

Akisimulia tukio hilo, bibi huyo (jina lihifadhiwa) alisema Novemba 5, 2023 jioni alimtuma mjukuu wake kwenda kumtafutia usafiri wa bodaboda lakini akashangaa baada ya kurudi akamwambia amebakwa.

"Mjukuu wangu huyu ambaye ni yatima, niliogopa sana kusikia amebakwa nikamuuliza mara ya pili na tatu, akasema ni kweli, kwenda kumchunguza nikakuta ni kweli ameingiliwa na amekuwa mwekundu sana sehemu za siri na amevimba,” amedai bibi huyo.

Amesema baada ya kuthibitisha hilo, alimpeleka hospitalini na baada ya kupimwa ilibainika ameingiliwa.

"Nilipewa PF3 Kituo cha Polisi Tengeru na kesi ikaenda mahakamani na mashahidi wote na ushahidi ukatolewa kwa ushirikiano mkubwa, lakini baadaye utetezi wake mtuhumiwa akanigeuka eti, nilikuwa namtaka na alivyokataa nikampa kesi hiyo,” amedai bibi huyo na kuongeza.

"Baada ya utetezi wake huo, Mahakama ilimuamini na kutupilia mbali ukatili aliofanyiwa mjukuu wangu akapewa ushindi.”

Alidai mbali ya mjukuu wake, wapo pia watoto wengine wanne ambao amedai walifanyiwa kitendo hicho na mtu huyo kwa nyakati tofauti.

Akizungumza katika mkutano huo, Makonda alimtaka Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arumeru kwa kushirikiana na wanasheria wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) na wataalamu wa afya kuhakikisha wanafufua jalada hilo.

"Ushahidi uko wa aina mbili, ikiwamo wa daktari aliyethibitisha na kutoa dawa, hivyo nendeni mkafufue upya jalada hilo na kesi ianze upya chini ya mawakili wetu wa TLS," amesema Makonda.

Mbali na hilo, amemtaka Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arumeru kuhakikisha wanamkamata mtuhumiwa huyo na kumfikisha polisi ili taratibu za kisheria zianze.

Mtoto asimulia

Akizungumzia tukio hilo, mtoto huyo amesema siku hiyo akiwa ametumwa na bibi yake kumtafutia usafiri wa bodaboda ndio alikutana na kadhia hiyo.

"Bibi yangu alinituma kumtafutia usafiri wa bodaboda barabarani, wakati naenda nikapita karibu na nyumba ya Babu Mchome akaniita akasema anataka kunituma niingie ndani kwake anichukulie hela,” amesema mtoto huyo.

"Kwa sababu babu ni mtu mzima, sikuwa na hofu nikaingia ndani kwake nikashangaa ananivutia kitandani kwake akanivua nguo na yeye akavua akaanza kuniingilia,” amedai mtoto huyo.

Amedai wakati anafanyiwa kitendo hicho alijaribu kupiga kelele lakini alizibwa mdomo hadi akamaliza haja yake.

Amedai baada ya hapo alikimbia kurudi nyumbani na kumueleza bibi yake kuwa amebakwa na alipomchunguza aligundua ni kweli ndipo akampeleka hospitali kupimwa na kugundulika kuwa kaingiliwa akapewa dawa za kumeza.

Chanzo: Mwananchi