Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wamuua mtuhumiwa wakidai alitaka kuwatoroka

Tue, 17 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sumbawanga. Mtuhumiwa wa ujambazi mkoani Rukwa ameuawa na polisi, ikielezwa alikuwa akijaribu kutoroka alipokuwa anakwenda kuwaonyesha wenzake walipo.

Taarifa ya polisi inasema mtuhumiwa alikuwa akitafutwa muda mrefu kutokana na kujihusisha na uhalifu wa kutumia silaha katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi.

Kamanda wa polisi mkoani Rukwa, George Kyando alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa Patrick Steven Kamagali (41) maarufu Mapinduzi, mkazi wa kitongoji cha Kashai kata ya Senga, Manispaa ya Sumbawanga.

Kyando alisema mtuhumiwa alikamatwa Julai 15 katika mji mdogo wa Laela akidaiwa kusafirisha risasi 30 za bunduki aina ya AK-47 kuelekea mkoani Mbeya.

Alisema baada ya kubanwa na askari mtuhumiwa aliahidi kwenda kuonyesha wenzake maeneo ya Senga, ambako ilibainika alichimbia SMG yenye namba 56- 3806320 na magazini yenye risasi 30.

Kamanda huyo alisema baada ya kuwaonyesha silaha, mtuhumiwa aliwaahidi kwenda kuwaonyesha wenzake anaoshirikiana nao kufanya matukio ya uhalifu na wakiwa njiani alijaribu kuwatoroka, hivyo askari walimpiga risasi na kufariki dunia papo hapo.

Mtuhumiwa anadaiwa kufanya matukio ya uhalifu zaidi ya saba katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe, Katavi na Kigoma.

Kyando alisema miongoni mwa matukio hayo ni lililotokea mkoani Rukwa mwaka 2002 katika kitongoji cha Malangali, Manispaa ya Sumbawanga kwenye kizuizi cha barabarani ambako akiwa na wenzake walimpiga nondo kichwani polisi na kumpora SMG.

Alisema baadaye alikamatwa na kufunguliwa kesi ambako mahakama ilimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 10 jela na kwamba, baada ya kutumikia adhabu hiyo alipotoka aliendelea na uhalifu.

Kamanda Kyando alisema polisi inaendelea kuwasaka watuhumiwa aliokuwa akishirikiana nao kufanya uhalifu, huku akiwaomba wananchi wenye taarifa zao kushirikiana na polisi na itawalinda.

Chanzo: mwananchi.co.tz