Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi waliokuwa wakisindikiza mitihani wakwama saa kadhaa Sumbawanga

1fadfb233460e1413fd75ad7d37ad276 Polisi waliokuwa wakisindikiza mitihani wakwama saa kadhaa Sumbawanga

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAOFISA Polisi waliokuwa wakisindikiza mitihani ya kitaifa wa kidato cha nne, walishindwa kuvuka Daraja la Mto Muze lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kwa saa kadhaa, kutokana na kusombwa na mafuriko ya maji.

Askari hao walikuwa wakisafirisha mitihani hiyo, iliyokuwa imefanywa tayari na wanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Mazoka . Mitihani hiyo ilikuwa inapelekwa kwa Kamati ya Mitihani ya Wilaya ya Sumbawanga.

Akipohojiwa na HabariLeo kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Kalolo Ntila alithibitisha mkasa huo.

Wanafunzi waliokuwa wakirejea nyumbani baada kufanya mtihani huo, nao pia walishindwa kuvuka. Walilazimika kusubiri kwa saa kadhaa hadi maji hayo yalipopungua. Alisema mkasa huo ni wa Desemba 2 mwaka huu mchana.

"Daraja hilo lilikatika siku nyingi ...mvua zilizonyesha kwa wingi Desemba 2 zilisababisha mafuriko ya maji yaliyolisomba pamoja na mawe yaliyokuwa msingi wa daraja hilo” alisema.

Akifafanua, Ntila ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Muze alisema kuwa madaraja mawili ya Muze na Uzia, yamesombwa na maji kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha. Mvua hizo zimesababisha walimu na wanafunzi, kushindwa kwenda shule.

Ofisa Elimu Mkoa wa Rukwa, Abel Ntupwa alikiri kutokea kwa mkasa huo. Hata hivyo, alisisitiza kuwa mitihani hiyo ilifikishwa salama na kukabidhiwa Kamati ya Mitihani ya Wilaya.

"Siku hiyo wanafunzi walimaliza kuandika mitihani hiyo saa tano asubuhi. Waliokuwa wakiisafirisha walichelewa kidogo, wakakuta daraja limejaa maji, lakini baada ya saa mbili walivuka salama" alisisitiza.

Aliongeza kuwa mkasa kama huo ulitokea mwaka jana katika Shule ya Sekondari Nankanga, ambayo mwaka huu imekuwa Kituo cha Mitihani.

"Mwaka huu tumechukua tahadhari ya kuifanya Shule ya Sekondari Nankanga kuwa Kituo cha Mitihani, maana yake mitihani inahifadhiwa kituoni hapo, kuna ulinzi na usimamizi wa kutosha” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz