Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amefuatana na wataalamu wakiwemo wa ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Ofisa Ustawi Wilaya ya Magu kuchunguza tukio la mtoto anayedaiwa kufa, kuzikwa na baadaye kuonekana akiwa hai.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa mtoto Mabilika Wilson (8) aliaga dunia Aprili 16 mwaka huu katika kijiji cha Salong’we, Kata ya Mwamabanza, Wilaya ya Magu na maziko yalifanyika kesho yake.
Alisema Aprili 27 mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni, mtoto huyo aliripotiwa kuonekana katika Kijiji cha Mwangika, Kata ya Mwabomba, Tarafa ya Ngulla, Wilaya ya Kwimba baada ya vijana waliokuwa wanachunga ng’ombe kumuona akiwa anahangaika porini peke yake.
Mtoto huyo alitoa ushirikiano kwa kujieleza kwao ni wapi, ambapo baada ya taarifa kufika polisi, askari wakazifanyia kazi kwa kumtafuta baba wa mtoto aitwaye Wilson Bulabo (35) na mama yake mzazi Helena Robert (33) wilayani Magu.