Mbeya. Polisi mkoani Mbeya linawashikilia viongozi 13 wa Soko la Sido jijini humo hatua ambayo imewafanya wafanyabiashara wa soko hilo leo Oktoba 10, 2018 kuyafunga maduka yao wakishinikiza kuachiwa kwa viongozi wao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema viongozi hao wanatuhumiwa kwa kosa la kuwazuia watumishi wa Serikali wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kufanya kazi ya kubandika namba kwenye maduka yaliyopo sokoni hapo.
Aliwataja viongozi hao kuwa ni mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Charles Syonga, na wengine ni Joyce Mwakyembe, Zedekia Athman, Modesta Sakyambo, Anna Philemon na Mary Leonard.
Wengine ni Augustine Paul, Leonard Philemon, Filiston Mwasomola, Jackson Mwakila, Osea Mwaisyelage, Dominick Bilali na Erick Ambile.
Kamanda Matei amesema chanzo cha tukio hilo ni wafanyabiashara hao kupinga kutoa ushuru wa pango la kila mwezi ambalo hukusanywa na watumishi wa Jiji la Mbeya kwa kila mfanyabiashara hapo sokoni.
Amesema upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
Kutokana na viongozi hao kushikiliwa, maduka yamefungwa huku wafanyabiashara na wale wanaojipatia ajira ya kubeba mizigo wakirandaranda nje ya maduka na wengine wakiwa kwenye vikundi wakijadiliana.
Wakizungumza na Mwananchi sokoni hapo, wafanyabiashara hao wamesema, jana walipata taarifa za viongozi wao kwamba wameitwa kwa mkuu wa wilaya ya Mbeya, Puali Ntinika lakini baadaye walipata mrejesho kwamba wamewekwa mahabusu na hawajui sababu.
Mfanyabiashara Charles Mgaya amesema, “Hatuwezi kufungua maduka yetu na tukaendelea na biashara wakati viongozi wetu wapo ndani na mbaya zaidi hatuelewi sababu ya kukamatwa kwao na kuwekwa ndani.”