Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi waimarisha ulinzi Pasaka

885029e794c09595946031edff44fb92.jpeg Polisi waimarisha ulinzi Pasaka

Fri, 2 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JESHI la Polisi limetangaza kuwa hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari na limejipanga kuhakikisha wananchi wanasherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa amani na utulivu.

Taarifa ya jeshi hilo kwa vyombo vya habari imebainisha kuwa, kwa siku tatu za kusherehekea Pasaka kuanzia Ijumaa Kuu, Jumamosi na siku ya kufufuka kwa Yesu Kristo yaani Jumapili, wananchi wawe huru kukusanyika na kusherehekea bila wasiwasi.

Taarifa hiyo ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime iliyataka makanisa, nyumba za ibada na mahala pengine ambako kutakuwa na mikusanyiko ya watu, kutoa ushirikiano kwa Polisi kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria vya uhalifu na uvunjifu wa amani.

”Kwa kuwa Ijumaa (leo) ni siku ya kifo cha Mwokozi Yesu Kristu, Wakristu hukusanyika katika nyumba mbalimbali za ibada kuomba, niwahakikishie usalama wao kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kuimarisha ulinzi kuanzia siku hiyo hadi siku ya Jumapili ambayo ndiyo sikukuu yenyewe ya Pasaka,” ilisema taarifa ya Misime.

Alisema ni kawaida kwa Jeshi la Polisi kulinda nchi, lakini wakati wa sikukuu ulinzi huimarishwa.

Msemaji huyo polisi alitoa mwito kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto, kuongeza umakini katika matumizi ya barabara hasa kuepuka kuendesha magari au pikipiki wakiwa wamelewa na kuepuka kuendesha vyombo hivyo kwa mwendo wa kasi.

Aliwataka watumiaji wote wa pikipiki kuvaa kofia ngumu na kutopakizana kwa idadi kubwa kuliko inayotakiwa kwa kuwa watakuwa wanahatarisha maisha yao.

Misime alisema makamanda wa vikosi mbalimbali wamejipanga kuhakikisha kunakuwa na amani na pia, wakuu wa usalama barabarani kwenye mikoa wamejipanga kukabiliana na viashiria vinavyosababisha athari za usalama barabarani.

“Askari wa vikosi vyote vya Jeshi la Polisi wapo kamili kukabiliana na uhalifu uwe jinai au hata unaohusiana na masuala ya usalama barabarani, lengo ni kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao ikiwa ni pamoja na kusherehekea kwa amani sikukuu hii muhimu,” alieleza.

Chanzo: www.habarileo.co.tz