Neema Omari (16), mkazi wa Kijiji cha Kewanja Wilaya ya Tarime mkoani Mara amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mkoani Mara, akidaiwa kupigwa risasi miguuni na polisi.
Neema alifikishwa hospitalini hapo Machi 2, 2024 baada ya kupewa rufaa kutoka Hospitali ya Nyamwaga wilayani Tarime alikopelekwa akitokea katika Kituo cha Afya cha Nyamongo alikopelekwa kwa matibabu baada ya kujeruhiwa.
Akizungumza hospitalini hapo leo Machi 4, 2024, daktari wa kitengo cha mifupa, Elias Nguti amesema baada ya kumfanyia uchunguzi wa awali ilibainika binti huyo ana vipande vya chuma kwenye miguu yote miwili.
"Tulimfanyia upasuaji siku hiyohiyo tukafanikiwa kutoa kipande cha chuma kwenye mguu wa kulia na jana tukafanya tena tukaondoa kwenye mguu wa kushoto, hivi sasa anaedelea vizuri ingawa bado amelazwa hapa hospitalini," amesema Dk Nguti.
Akisimulia jinsi tukio lilivyotokea, mama mzazi wa mtoto huyo, Bhoke Chacha amesema tukio hilo lilitokea Februari 29, 2024 saa 12 jioni wakati akiwa njiani akirudi kwenye mgahawa wake alipokuwa amemuacha binti yake.
Amesema alimuacha mwanawe huyo mgahawani kwake eneo la Mrwambe katika Kijiji cha Kewanja ili asimamia kazi.
"Nilienda kwenye kikao cha kikundi na kumuacha Neema kwenye mgahawa nikiwa narudi, ghafla tukasikia kelele vijana wakawa wanakimbia, mara likapita gari moja likiwa na askari, wakafyatua risasi ambazo moja kwa moja ziliingia kwenye mgahawa wangu," amedai mama huyo.
"Na mimi nilivyoona vile, nikaanza kukimbia kuelekea kwenye mgahawa wangu na watu wengine wakawa wanelekea hapo, ghafla yakaja magari mengine manne ya maaskari wakafyatua tena risasi, watu wakaanza kukimbia kila mtu akijaribu kujiokoa, mimi nikafika kwenye mgahawa nikamkuta mtoto amelela chini huku akitokwa na damu nyingi," anasimulia mama huyo. Amedai chanzo cha askari hao kufyatua risasi ni kutokana na kudaiwa kulikuwa na vijana waliotaka kuvamia mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara kuokota mawe ya dhahabu.
“Na siku hiyo mvua ilinyesha na kawaida mvua zikinyesha kuna vijana huwa wanaingia mgodini kuokota mawe na pale Mrwambe ni jirani na mgodi," amesema Chacha.
Neema alivyojeruhiwa Akieleza namna alivyojeruhiwa, Neema anasema akiwa mgahawani anakula chakula, ghafla walisikia mlipuko mkubwa nje ya mgahawa hali iliyomlazimu kukimbia na kufunga mlango.
"Nikiwa ninafunga mlango risasi ilipita kwenye uwazi wa mlango kwa chini na kunipiga kwenye miguu yote miwili hapo hapo nilianguka chini na sikujua kilichoendelea hadi nilipojikuta niko hospitalini," amesimulia Neema.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Tarime/Rorya, Mark Njera alipotafutwa azungumzie tukio hilo, simu yake haikupokewa na alipotumiwa ujumbe wa maneno, amejibu kwa ufupi, “niko kikaoni nitatoa taarifa kwenu juu ya tukio hili."