Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wabaini mtandao wa wauaji wa watoto

40149 Pic+mauaji Polisi wabaini mtandao wa wauaji wa watoto

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Njombe. Jeshi la Polisi mkoani hapa limesema limebaini mtandao wa watu wanaotekeleza utekaji na mauaji ya watoto wadogo kisha kuwatupa porini wilayani Njombe.

Mbali ya kubaini mtandao huo, tayari watu 28 wakiwamo waganga wa jadi sita, wafanyabiashara na watu wa kawaida wanashikiliwa na polisi kuhusiana na matukio hayo.

Katika matukio hayo yalianza kuibuka Novemba mwaka jana, watoto wa shule za msingi wamekuwa wakitekwa na kuuawa, kisha kutupwa porini na wengine hawajulikani walipo tangu walipotoweka.

Jana, akizungumzia hatua zinazoendelea kuchukuliwa na msako wa mtandao unaohusika na mauaji ya watoto wilayani Njombe, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Renata Mzinga alisema:

“Wananchi wa Njombe waendele kutupa ushirikiano, tumeshapata mtandao wa watu waliokuwepo na wametekeleza mauaji hayo, hivyo tunaendelea kushirikiana na wenzetu wa mikoa jirani ili tuhakikishe tunatokomeza makundi haya maovu. Lakini tunazo taarifa na tutawakamata hukohuko waliko kuhakikisha mkoa wetu upo shwari na nchi kwa ujumla.

“Hatuwezi kuacha (wahalifu) wakaendelea kuteketeza roho za watu. Sio Njombe pekee, bali hata mikoa mingine. Ndio maana tunasema kule waliko tumefahamu tutawafuata tu.”

Akifafanua kuhusu msako huo, kamanda huyo alisema kuna wageni waliingia Njombe kwa kisingizio cha kuwa ni waganga wa jadi lakini kamatakamata ilipoanza, walikimbia kwa vile walikuwa wakiendesha uovu lakini bado tunawafuatilia hukohuko waliko.

Kamanda Mzinga alisema pamoja na kuwashikilia washukiwa hao 28, pia walimhoji ofisa afya wa Mkoa wa Njombe, Mathias Gambishi ambaye alikuwa mratibu wa kutoa leseni za waganga wa jadi.

“Tulimuita (Gambishi) tulimhoji na tukamuachia. Ametusaidia ya kwake lakini tutaendelea kumhoji ili aweze kutupa mwongozo hasa kwenye uhakiki wa waganga wa jadi katika mkoa wetu wa Njombe,” alisema

Kamanda Mzinga alisema hadi sasa jeshi hilo limefanya uhakiki wa leseni za waganga 50.

Alisema hadi sasa mtoto mmoja Gaudence Kihombo (7) mkazi wa Kijiji cha Ikando Kata ya Kichiwa bado hajulikani alipo tangu apotee Januari 6 na kwamba uchunguzi unaendelea.



Chanzo: mwananchi.co.tz