Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo, amesema wamejipanga vyema kukabiliana na dawa za kulevya pamoja na vilipuzi vya aina yoyote.
Ametoa kauli hiyo mjini hapa, leo Agosti 12, 2022, alipotembelea kikosi cha mbwa na farasi kwa ajili ya kukagua mazoezi maalum ya mbwa wanaotumiwa na jeshi hilo kuwatambua wahalifu mbalimbali, wakiwemo wa dawa za kulevya, silaha na mabomu.
Amesema kupitia kikosi hicho pia wanatoa mafunzo kwa mbwa wa kiraia, ili kuimarisha ulinzi na usalama mkoani Arusha.
Kwa upande wake mkuu wa kikosi cha mbwa na farasi mkoa wa Arusha, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), William Mwaisumo amesema wamejipanga vyema kutoa mafunzo kwa mbwa wote wataopelekwa kupata mafunzo ya ulinzi na utambuzi wa dawa na vilipuzi.