Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi aeleza walivyouopoa mwili mtoni ukiwa umeanza kuharibika

50409 POLIS+PIC

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Shahidi wa pili wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Scolastica ameeleza namna walivyouopoa mwili wa mtoto huyo katika mto uitwao Ghona.

Mwanafunzi huyo, Humphrey Makundi, anadaiwa kuuawa na watu wasiojulikana Novemba 6, 2017 na mwili wake kutupwa katika mto huo uliopo takribani mita 300 kutoka shule hiyo iliyopo kwenye mji wa Himo.

Shahidi wa pili wa mashtaka, Koplo Augustino alitoa ushahidi wake huo juzi mchana mbele ya Jaji Firmin Matogolo wa Mahakama Kuu anayesikilizia kesi hiyo katika Mahakama Kuu mjini hapa.

Akiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula kutoa ushahidi huo, askari huyo aliungana na shahidi wa kwanza, Dk Alex Mremi, aliyeeleza mwili wa marehemu ulianza kuharibika.

Katika ushahidi wake huo, shahidi huyo alidai kuwa Novemba 10, 2018 alipigiwa simu na mkuu wake wa kazi na kumtaka arudi kituoni Himo, na alipofika alimweleza juu ya kuonekana kwa mwili huo. “Nilienda ofisini tukachukua fomu na machela tukapanda gari ya polisi, tulienda mpaka shule ya Scolastica tukapaki gari tukatembea kwa mguu nikiwa nimeongozana na kiongozi wangu,” alidai.

“Tukiwa tunaelekea eneo la tukio njiani tulikutana na watu wanne na kati ya hao mmoja wao ndio aliyempiga simu kiongozi wangu.”

Augustino alidai, “(mtu huyo) alituongoza mpaka eneo la tukio na tulipofika tulikuta mwili wa kijana huyo ukielea kwenye maji (ya mto Ghona) ukiwa umeharibika”

“Tulikuta mwili wa jinsia ya kiume ukiwa umevaa bukta, tshirt na soksi ukiwa unaelea huku ukiwa umelala kichwa kimeinamia chini. Tuliuchukua na kuugeuza, tulibaini ni mtoto wa kiume.”

Shahidi huyo alidai, “tulichukua mwili huo kwenye machela tukaenda nao kituoni ndipo baadaye tulienda moja kwa moja hadi hospitali ya Mawenzi kuhifadhi mwili kwa ajili ya taratibu nyingine za kiuchunguzi kuendelea.”

Akitoa ushahidi huo, askari huyo wa kitengo cha upelelezi alidai licha ya mwili huo kuondolewa kwenye maji sehemu ya fuvu katika paji la uso kulikuwa na jeraha kubwa.

Ushahidi huo unashabihiana na wa Dk Mremi ambaye ni daktari bingwa wa patholojia katika hospitali ya KCM alioutoa juzi, akisema katika uchunguzi walibaini uwepo wa jeraha kubwa kichwani.

“Mwili ulikuwa na majeraha na tulibaini jeraha kubwa kwenye paji la uso lililovunja fuvu la kichwa. Jeraha hilo tulipolipima lilikuwa na ukubwa wa sentimeta 6 kwa 5,” alidai daktari huyo katika ushahidi alioutoa mahakamani hapo.

“Chanzo cha kifo ni uwepo wa jeraha kubwa lililovunja mfupa. Ni jeraha lililosababisha kifo. Mwili ule ulikuwa ni wa mtoto wa kati ya miaka 15 na 17 kutokana na mwonekano wa meno.”

Alidai, “yalikuwepo na majeraha mengine ambayo ni michubuko mabegani, mgongoni na mapajani. Tulichukua pia mifupa mbalimbali na nyama kwa ajili ya kufanya DNA (vinasaba).”

Kesi hiyo inayoendeshwa na jopo la mawakili wanne wa Serikali wakiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Joseph Pande itaendelea tena leo kwa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wake.



Chanzo: mwananchi.co.tz