Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi: Tumejipanga kupambana na biashara ya bidhaa bandia

39900 FCC+pic Polisi: Tumejipanga kupambana na biashara ya bidhaa bandia

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Jeshi la Polisi nchini limesema limejizatiti ipasavyo katika kupambana na biashara ya bidhaa bandia kama sehemu ya kusaidia nchi kufikia uchumi wa kati na viwanda.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na mkuu wa mitalaa ya Jeshi la Polisi nchini Fulgence Ngonyani kwenye ufunguzi wa mafunzo kwa maofisa upelelezi wa makosa ya jinai wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na wilaya yaliyoandaliwa na Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) yaliyokuwa na lengo la kuwajengea uwezo maofisa hao kupambana na biashara ya bidhaa bandia.

Ngonyani alisema makosa ya bidhaa bandia ni makosa ya jinai na kwamba kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia makosa haya yanahusiana kwa kiasi kikubwa na makosa ya uhalifu wa kifedha.

Alisema biashara ya bidhaa bandia ni kubwa ulimwenguni hivyo mamlaka za kiserikali pamoja na polisi hawana budi kushirikiana kupambana na janga hilo.

Akizungumza katika semina hiyo, mkuu wa mkoa wa Mbeya Albert Chalamila, aliwataka maofisa hao kutumia mafunzo hayo kuwa chachu ya kufanya kazi kwa ufanisi na uadilifu bila kukata tamaa.

"Ukiona uhalifu unaendelea haina maana kwamba polisi wameshindwa ila ipo siku utakoma kwani uadilifu haujengwi kwa siku moja," alisema Chalamila.

Chalamila alisema bidhaa bandia zimekuwa zikileta hasara katika uchumi wa Taifa kutokana na wafanyabiashara hiyo kukwepa kulipa kodi jambo linaloirudisha nchi nyuma kimaendeleo.

Kwa upande wake, mwakilishi wa mkaguzi mkuu na mkurugenzi wa FCC, Magdalena Utouh alisema kukua kwa uchumi wa Nyanda za Juu Kusini kunaweza kuchochea kuwepo bidhaa bandia hivyo semina hiyo itasaidia maofisa hao kujua namna ya kukabiliana na tatizo hilo.

"Jeshi hili lina jukumu la kushughulikia uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka dhidi ya makosa yanayohusiana na bidhaa bandia, hivyo kulijengea uwezo jeshi hilo ni jambo muafaka katika jitihada za kudhibiti bidhaa bandia," alisema Utouh.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz