Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Tanzania yawataka wanaoishi mabondeni Dar kuhama

88942 Polis+pic Polisi Tanzania yawataka wanaoishi mabondeni Dar kuhama

Wed, 18 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa tahadhari kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni na kuwataka kuondoka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Jumanne Desemba 17, 2019 wakati wa doria ya kutathimini ya athari zilizotokana na mvua, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Juma Ndaki amesema maeneo ya bonde la Mto Msimbazi hali ni tete hivyo kuwataka wananchi kuchukua tahadhari kwenye maeneo hayo.

“Athari kubwa iko Msimbazi, hali ni tete, tushikilie msimamo wa Serikali yetu kuwa wote walioko kwenye mabondeni wanatakiwa watoke, imefika wakati sio muda wa kuwabembeleza ni kuwatoa kwa nguvu” amesema Kamishna Ndaki

Amesema maeneo mengine ambayo bado ni hatarishi ni pamoja na maeneo ya Jangwani na barabara ya kuelekea Kigogo.”

“Tunatoa tahadhari kwa ambao wanataka kupita kwenye maeneo hatarishi, wasipite kwenye maeneo hayo.”

Amewataka wananchi ambao wanaishi maeneo hatarishi waondoke ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kujitokeza

Doria hiyo ya angani ambayo imefanywa na helikopta ikiongozwa na kamishna Ndaki imepitia maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ikianzia uwanaja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, bonde la mto Msimbazi, Kigamboni, Kigogo na Kariakoo.

Maeneo mengine waliyopita kufanya tathimini ni; Kawe, Tegeta, Sinza na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo maeneo haya hayakuwa na athari kubwa.

Kamishna Ndaki amewataka wananchi kuchukua tahadhari ambapo jeshi hilo litaendelea kufanya tathimini nyingine baadaye na kutoa taarifa ya madhara ambayo yamejitokeza.

Mvua hizo ambazo zilianza kunyesha majira ya asubuhi leo Jumanne Desemba 17, 2019 zimesimamisha shughuli za kiuchumi na kijamii na kusababisha adha ya usafiri kwa wananchi.

Chanzo: mwananchi.co.tz