Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Moshi wadaiwa kuua mtuhumiwa kwa kipigo

Mtuhumiwa Polisi Moshi wadaiwa kuua mtuhumiwa kwa kipigo

Fri, 14 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Kilio cha washukiwa wa uhalifu kufariki mikononi mwa polisi, kinazidi kulitikisa Jeshi la Polisi, baada ya kutokea tukio mkoani Kilimanjaro, kwa mkazi wa Kijiji cha Mvuleni Newland, Wilaya ya Moshi, Joseph Zakayo, kudaiwa kuuawa kwa kipigo.

Taarifa kutoka kwa baadhi ya ndugu na kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zinadai kuwa mtuhumiwa huyo wa wizi wa televisheni ya mmoja wa askari wa jeshi hilo, alipigwa baada ya kukamatwa na kumshinikiza akubali kutenda kosa.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alipigwa nyumbani kwa askari na baadaye alipelekwa hospitali ya Kiwanda cha Sukari cha TPC ambapo walielekeza awahishwe Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Juni 4, 2024 nyumbani kwa askari hao, baada ya marehemu na wenzake kukamatwa wakituhumiwa kwa wizi ambapo baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi, Zakayo alipoteza Maisha.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Simon Maigwa alipotafutwa na Mwananchi leo Alhamisi Juni 13, 2024 azungumzie tukio hilo, hakukanusha wala kukiri, lakini amesema yuko nje ya ofisi na kuomba mwandishi wa habari amuone kesho Juni 14, ili aweze kulizungumzia.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mvuleni Wilaya ya Moshi, Salim Yahaya alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, amekiri vijana hao kupigwa nyumbani kwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ambako ndiko kulidaiwa kuibiwa TV.

Yahaya amedai kulifahamu tukio hilo la wizi lililotokea nyumbani kwa askari ambao ni mume na mke na waliendelea kuwatafuta wahusika lakini walipokamatwa hakupewa taarifa hadi alipojulishwa kupigwa vijana kadhaa na mmoja kufariki.

“Nilikuwa na taarifa za kuibiwa TV kwa hao askari, lakini siku wanawakamata hawakunipa taarifa, nilikuja tu kupewa taarifa wamewakamata na kuwapiga na wamelazwa hospitali. Walipigwa nyumbani kwa askari ambao ni mume na mke,” ameeleza.

Mwenyekiti huyo ameongeza kusema; "Walipowakamata saa mbili kwenda saa tatu usiku hawakuniambia, ila kwenye saa nane usiku, alinipigia simu huyo mmoja wa maaskari akiniambia watuhumiwa wamekamatwa na wako kituo cha polisi."

"Nilipofuatilia kituo cha Polisi TPC nilipewa taarifa kuwa walipelekwa wakiwa na hali mbaya na walipelekwa hospitali na baadaye kidogo nikapewa taarifa huyu kijana mmoja amefariki," ameeleza mwenyekiti huyo alipozungumza na Mwananchi Digital.

Ndugu wa marehemu asimulia

Akisimulia tukio hilo, ndugu wa marehemu, Samuel Enos amedai siku ya tukio alipigiwa simu akielezwa kuwa ndugu yake anapigwa akituhumiwa kuiba, alipokwenda eneo la tukio alimkuta ndugu yake akipigwa na yuko na hali mbaya.

Samuel ambaye alikuwa akiishi na marehemu amesema; "Niliuliza tatizo ni nini, nikaambiwa ni mwizi, nikawaambia kama ni gharama naomba mumuache mimi nitalipa na walikuwa wakipigwa vijana wawili, ndugu yangu na kijana mwingine.”

"Nilimsogelea ndugu yangu kumuuliza nini kimetokea, akaniambia siyo kweli wanamsingizia, lakini wakati akinieleza hivyo, wale waliokuwepo wakamsonga na kusema anasema uongo," ameeleza ndugu huyo wa marehemu. Polisi Moshi wadaiwa kuua mtuhumiwa kwa kipigo

Kwa mujibu wa ndugu huyo wa marehemu, alidai kuwa vijana hao wakati wanapigwa, walikuwa wamefungwa kamba nyuma huku wakiwa wamevuliwa nguo na kubaki na bukta na kila wakipigwa walikuwa wanamwagiwa maji.

"Wakati naongea nao nipate mwenye nyumba hiyo ambako tukio linatokea ni nani ili nizungumze naye, niliambiwa mwenye nyumba ni askari, mume ni askari na mke ni askari,” amefafanua Enos.

"Wakati nauliza hivyo nikaona bajaji imeingia wakaambiwa wavae nguo zao zikiwa zimeloa na kupakizwa kwenye bajaji ambapo niliungana nao tukaenda hadi Kituo cha Polisi TPC na wakati huo ilikuwa saa 8 usiku,” alidai ndugu huyo.

"Polisi aliyetupokea alihoji kwa nini wamepigwa kiasi hicho, akauliza kama wana RB nikasema sijui, akasema hata kama ni watuhumiwa hawezi kuwaingiza ndani kwa hali walivyo kwa kuwa wana hali mbaya labda waandike PF."

"Wakati wakitaka kuandika PF3 hiyo, askari yule alipokea simu, na mimi nilikuwa na mdogo wangu ameniegemea, lakini baada ya polisi kumaliza kuongea nilivutwa shati na kuingizwa mahabusu polisi pamoja na mwenye nyumba wangu niliyeenda naye pamoja na dereva bajaji na kumuacha ndugu yangu na yule kijana mwingine pale," amesimulia.

Alieleza kuwa, “Asubuhi niliitwa nikafungwa pingu na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Moshi Mjini, tukabaki kuulizana imekuwaje tuwekwe ndani lakini tukiwa pale tulisikia mmoja wa waliopigwa amefariki kwa kuwa alikuwa amejeruhiwa sana."

"Nililala tena polisi na Alhamisi saa sita niliachiliwa sijui nini kilitokea wala nani alinidhamini. Hivyo niko huru mpaka leo lakini nilipotoka nilianza kufuatilia kumtafuta ndugu yangu. Nilianza KCMC lakini sikuweza kumpata huko.”

Alidai alipitia wagonjwa wote walioingia kama wagonjwa na waliofariki lakini hakumuona ndugu yake hivyo akashauriwa arudi polisi kujua walikompeleka.

"Nilirudi polisi kuuliza wakaniambia hayuko KCMC yuko Mawenzi, nikaja Mawenzi lakini muuguzi niliyemkuta akasema jina hilo hayupo, ikabidi nianze kukagua mwili mmoja baada ya mwingine mochwari hadi nilipokutana na mwili wa ndugu yangu," amesimulia.

Amedai baada ya kuupata mwili wa ndugu yake taratibu, ulipelekwa KCMC kwa ajili ya uchunguzi na baadaye kurudishwa Mawenzi ambako alidai uchunguzi ulibainisha amepigwa kichwani na damu ilivia kwenye ubongo.

Wazuiwa kuchukua mwili

Akielezea kuzuiwa kuchukua mwili, ndugu huyo amedai leo Juni 13, 2024 walifika Hospitali ya Mawenzi kwa ajili ya kuchukua mwili kwenda kuzika lakini wakati wakiendelea na taratibu za kuchukua mwili kwa ajili ya mazishi.

Hata hivyo, alidai kuna simu ilipigwa na askari mmoja akiwaeleza hawawezi kuchukua mwili kwa kuwa wanapaswa kuusafirisha kwenda kuzika mkoani Kigoma ambako ndiko nyumbani kwa marehemu na siyo eneo ambalo alikuwa akiishi.

"Nilishindwa kuelewa maana mwanzo tulitaka kusafirisha tukazike nyumbani Kigoma, tukawa hatuna hela, tukaomba msaada polisi, tuliambiwa hakuna utaratibu wa kusafirisha mwili wa mtuhumiwa ndipo tukaamua tutazika Newland."

"Wakati huo tayari ndugu zetu akiwemo mama Mzazi akasafiri kuja kwa maziko. Suala la kuzuiwa kulitushtua sana.”

"Lakini baada ya kuambiwa hivyo niliwajulisha wenzangu ambao wengine walikuwa wamefuata jeneza, tukaenda kwa mkuu wa wilaya, tunashukuru ametusaidia na sasa tunauchukua mwili kwenda kuupumzisha Newland,” amesema.

Chanzo: Mwananchi