Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Manyara waokoa zaidi ya Sh47 milioni

Pesa Fedhaddd Polisi Manyara waokoa zaidi ya Sh47 milioni

Fri, 9 Jun 2023 Chanzo: mwanachidigital

Jeshi la Polisi mkoani Manyara linawashikilia watu wawili, Juma Athumani (23) na Mariam Mbega (26) kwa tuhuma za kuvunja nyumba na kuiba Sh47 mil za Laurent Elias mfanyabiashara na mkazi wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.

Baada ya uhalifu wa kuiba fedha hizo watuhumiwa walizificha benki kwenye akaunti zao ili wasibainike na kukamatwa.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, ACP Goerge Katabazi leo Juni 9, 2023 amesema tukio hilo lilitokea Juni 6, 2023 katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.

Amesema Jeshi la Polisi limezuia fedha hizo zisitoke benki ili taratibu za kisheria zifuate na kwamba watuhumiwa wanashikiliwa kwa upelelezi zaidi.

"Tumezuia fedha hizo zisitoke benki na tunaendelea na upelelezi...Lakini kwa ushahidi tuliokusanya mazingira na vielelezo ni huenda watuhimiwa wamehusika na wizi huu kwa fedha ambazo nimezitaja ambazo ni zaidi ya Sh47 mil," amesema ACP Katabazi.

Amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa operesheni zinazofanywa na jeshi hilo la Polisi ambapo wiki mbili zilizopita waliokoa zaidi ya Sh20 milioni za mmoja wa wafanyabiashara mjini babati.

"Huu ni mwendelezo wa kudhibiti matukio ya wizi mkoa wa Manyara, wiki mbili zilizopita pia tuliokoa zaidi ya Sh20 mil za mmoja wa wafanyabiashara mjini Babati," amesema ACP Katabazi.

Kamanda Katabazi ametoa wito wa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wa kuwafichua wahalifu… "Tunaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kuendeleza dhana ya ulinzi shirikishi pamoja na ulinzi jirani…wawe na vikundi vya ulinzi shirikishi maeneo yao kwanzia kutongoji hadi mitaa ili kudhibiti uhalifu huo," amesema.

Amesema sheria haimkatazi mtu kuwa na kiwango kikubwa cha fedha lakini awe na tahadhari na kutoa wito kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kuhifadhi fedha taasisi za kifedha ili ziwe salama zaidi.

"Wakati mwingine kuwa na kiwango hicho cha fedha bila kuweka benki huwa ni kivutio cha wahalifu. Nitoe rai kwa wananchi, mwenye fedha nyingi asiendelee kuwa nazo nyumbani kwake ni bora kuhifadhi benki," amesisitiza ACP Katabazi.

Aisha ACP Katabazi amesema kuokoa kiasi hicho cha fedha kinahitaji maadili na weledi wa kazi na sisi Jeshi la Polisi Manyara tumejipambanua tunafanya kazi kwa kuzingatia maadili na weledi wa kazi zetu.

Chanzo: mwanachidigital