Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi, Madereva na makondakta Tanga walalamikiwa na walemavu

Tue, 2 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Watoto wenye ulemavu Jijini Tanga, wamelilalamikia jeshi la polisi mkoani humo kwa kutowachukulia hatua watoa huduma wa usafiri wa umma (daladala) wanaokatisha safari na kutoa lugha za kuwanyanyapaa.

Watoto hao wamesema  licha ya kuwasilisha malalamiko yao mara kwa mara kwenye vyombo husika lakini matukio ya unyanyasaji kwa watoto na vijana wenye ulemavu kwenye daladala unaendelea na hivyo kujiona kuwa si sehemu ya jamii.

Wamebainisha hayo jana Jumamosi Juni 29, 2019, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya mtoto wa Afrika yaliyoandaliwa na kituo cha kulea watoto wenye ulemavu jijini Tanga (YDCP).

Mwanamvua Zumo amesema akiwa ndani ya daladala kondakta alipogundua kuwa ana ulemavu wa kushindwa kutamka vyema maneno alimpitilizisha kituo ambacho ilikuwa ashuke na kumzungusha mara mbili jambo lililosababisha achelewe kufika hospitali kutibiwa.

“Iliniuma sana nikaona kuwa nanyanyasika kwa sababu ya ulemavu wangu ,nililalamika sehemu mbalimbali lakini sikusikilizwa kabisa,” alilalamika Mwanamvua huku akitoa machozi.

Subira Bakari amesema matukio ya wenye daladala kukatisha safari ni ya kawaida jijini Tanga licha ya kuwasilisha malalamiko jeshi la Polisi na Sumatra lakini hakuna hatua zinazochukuliwa za kukomesha jambo hilo.

Pia Soma

Mtetezi wa haki za watoto wenye ulemavu wa kituo cha YDCP, Prisca Mwakasindile anasema matukio ya makondakta kuwatolea lugha mbaya watoto wenye ulemavu zimekithiri na kuomba vyombo husika viingilie kati kwa sababu zinawaathiri kisaikolojia.

 “Kuwaita majina kama Chenga, Zombi, Mtambo, taahira, Zeruzeru na kiwete zinawaathiri mno kisaikolojia hawa watoto, mara nyingi wanakuja hapa wakiwa wanalia na kulalamika kwamba kwenye daladala wanaitwa majina hayo,” anasema  Prisca ambaye pia ni mtaalamu wa kutafsiri lugha ya alama.

Mratibu wa dawati la jinsia wa jeshi la Polisi Wilaya ya Tanga, Yason Mnyanyi aliwafundisha watoto hao namna ya kuyakariri magari ambayo makondakta wao hujihusisha na unyanyasaji na jinsi ya kutoa taarifa vituo vya polisi.

“Malalamiko yote nimeyasikia niwaahidi tu kwamba tutayafanyia kazi, yale yanayohusu trafiki na Sumatra na mengine ambayo yanahusu moja kwa moja dawati tutashirikia na YDCP kuhakikisha yanakomeshwa,” amesema Yason.

Ofisa ustawi wa jamii wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Godfrey Akumo anasema ukatili unaoongoza kwa watoto wenye ulemavu kwa sasa ni wa kisaikolojia ukifuatiwa na kuwaadhibu kwa vipigo na kuwafungia ndani ya nyumba.

Chanzo: mwananchi.co.tz