Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Iringa yawashikilia wawili kwa kukutwa na magobore matano

Polisi Iringaaa Polisi Iringa yawashikilia wawili kwa kukutwa na magobore matano

Wed, 12 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Jeshi la Polisi mkoani Iringa linawashikilia watu wawili kwa tuhuma ya kukutwa na bunduki za kienyeji aina ya gobore tano wanazodaiwa kuzitumia kufanyia ujangili.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Kamishna Msaidizi, Alfred Mbena amesema watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni za mara kwa mara zinazoendelea kufanyika mkoani humo.

Watuhumiwa hao ambao ni Afya Kityega (47), mkazi wa Idodi na Fredy Lukosi (25) mkazi wa Kijiji cha Ugwachanya, baada ya kupekuliwa walikutwa na chupa mbili za baruti, kamba ya manila, rissington za gobore ambavyo ni vipande vya nondo na begi dogo jeusi.

Amesema watuhumiwa baada ya kuhojiwa wamekiri kuzitumia silaha hizo kutekeleza vitendo vya ujangili.

Wakati huohuo Jeshi hilo linamshikilia Thomas Ngoti (37) mjasiriamali na mkazi wa Mgera Kihwele mkoani Iringa akiwa na kofia, suruali moja, mkanda mmoja na begi ambazo ni sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ).

Amesema mtuhumiwa alikamatwa eneo la makazi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kata ya Gangilonga na baada ya kuhojiwa alidai kuwa nguo hizo ni mali yake na amewahi kuwa askari wa Jeshi hilo kabla ya kuacha kazi.

Katika tukio lingine, Polisi wanawashikilia watu watano wakiwa na vipande vinne vya meno ya tembo.

Amesema watuhumiwa wamekamatwa wakiwa kwenye mkakati wa kufanya biashara hiyo ndani ya nyumba moja ya kulala wageni eneo la Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo.

Kamanda Mbena amesema watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Chanzo: Mwananchi