Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi: Hatujabaini makaburi eneo la kanisa lililofungwa

Makaburi.png Polisi: Hatujabaini makaburi eneo la kanisa lililofungwa

Wed, 14 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza likiendelea kumshikilia William Masuma na mkewe, Kabula Lushika kwa tuhuma za kutoa huduma ya maombi kinyume cha sheria, uchunguzi wa awali haujagundua uwepo wa kaburi lolote katika eneo la kanisa walikokuwa wakiendesha ibada.

Masuma na mkewe Kabula, wakazi wa Kijiji cha Nyamhinza Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wanadaiwa kutoa huduma ya maombi kwa wagonjwa waliokutwa wamepewa huduma ya ‘kulazwa.’

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alisema kamati ya uchunguzi iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paulo Chacha inayoshirikisha vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali haijabaini uwepo wa makaburi katika maeneo ya makazi ya watuhumiwa hao.

Kamati ya kuchunguza sakata hilo inaundwa na wajumbe kutoka Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mganga wa Wilaya ya Misungwi, Idara ya Utamaduni na Ardhi wilayani Misungwi.

“Tunaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo ikiwamo mahojiano ya watuhumiwa. Nawaomba wananchi wenye taarifa zitakazosaidia uchunguzi wajitokeze,’’ alisema Kamanda Mutafungwa.

Pia, alisema katika uchunguzi wa awali, Jeshi la Polisi limebaini wawili hao sio tu hawakuwa na kibali cha kuendesha ibada na shughuli za maombi, bali pia hawakuwa na kibali cha kutoa huduma ya tiba asili tofauti na madai ya mtuhumiwa Masuma wakati huduma hizo zilipobainika Juni 9, mwaka huu.

Awali, Mhubiri Masuma kabla ya kupelekwa kituo cha polisi wiki iliyopita alidai kuwa, hakuna wagonjwa waliokufa katika eneo hilo kwa kuwazuia kwenda hospitali.

Alidai kuwa, anatoa huduma ya maombi kwa wenye imani na watapona kwa kuombewa.

Masuma alisema wito wa kufanya maombezi aliupata miaka 10 iliyopita baada ya kuugua ugonjwa usiofahamika na hakupona hospitalini, bali alipoombewa na mhubiri, ambaye pia alimweleza ana karama ya kuponya maradhi kwa kutumia maombi.

“Ninafanya maombi tu sitoi huduma ya matibabu hapa. Kuna magonjwa siwezi kuyatibu, mfano mtu akiletwa anaumwa ugonjwa wa kupungukiwa damu huwa namshauri aende hospitalini au kama ana malaria ninamshauri aende hospitalini.

“Nawapokea wagonjwa, nawapatia eneo wajenge nyumba wanayoweza kumudu kuishi na kuhusu fedha wanapofika wanatoa ka-hela kadogo kwa ajili ya huduma hiyo, nyingine wanatoa wakishapona. Kuhusu mtu kufa akiwa hapa sina taarifa,” alisema mhubiri huyo kabla ya kukamatwa.

Baada ya mkuu wa wilaya kutangaza kusitisha huduma, baadhi ya wagonjwa waliruka sarakasi, huku wakiangua kilio wakidai hawako tayari kuona huduma hiyo inasitishwa.

Maombi hayo hayakufua dafu, baada ya polisi kuingilia kati na kuwachukua kwenye karandinga na kuwapeleka katika Kituo cha Afya cha Misasi.

Chanzo: Mwananchi