Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Arusha yapiga marufuku disco toto, faTaki

33438 CHUGA.png Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Jeshi la polisi mkoa wa Arusha limepiga marufuku disco toto na upigaji ovyo fataki na risasi hewani katika maadhimisho ya sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.

 

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng'anzi akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Desemba 25, 2018 amesema polisi limechukua hatua hiyo ili kudhibiti matukio ya uhalifu mitaani hasa baada ya kuvuka salama bila tukio la uhalifu katika mkesha wa Krismasi.

 

"Tumepiga marufuku disco toto  na tabia ya kupiga risasi juu na fataki wakati wa sikukuu bila kufuata utaratibu," amesema.

 

Amesema ila kwa wale ambao watataka kupiga fataki wanapaswa kuwasiliana na viongozi wa mitaa na kutenga maeneo maalum ya wazi ambapo watu watakutana na kupiga fataki.

 

Hata hivyo, amesema jeshi hilo pia tayari limesambaza askari katika mitaa mbalimbali mkoani hapa ili kuhakikisha wanadhibitiwa wahalifu na akatoa wito kwa wazazi kuchunga watoto wao kutembea ovyo mitaani.

 

"Tumesherehekea salama mkesha wa Krismasi bila tukio lolote na tunataka hali hii iendelee hadi mwaka mpya hatutaki uhalifu wala ajali katika mkoa wa Arusha," amesema.

 

Kamanda Ng'azi pia amewataka wazazi wanaotoka majumbani kwenda matembezi kufunga nyumba zao lakini pia kuchukua tahadhari za kiusalama katika maeneo yao.

 

Wakizungumzia sherehe ya Krismasi baadhi ya wakazi wa Arusha, wameshukuru kuwepo kwa amani tofauti na miaka ya nyuma ambapo matukio ya uhalifu hutokea.

 

Saumu Adam, mkazi wa Arusha amesema wanalipongeza jeshi la polisi na wadau wengine kwa kuhakikisha Arusha inakuwa na amani na hivyo kuifanya sherehe  ya Krismasi kuwa ya utulivu.

 

"Tunaomba hali hii ya utulivu iendelee hadi mwaka mpya kwani Arusha sasa ni shwari tofauti na miaka ya nyuma," amesema.

John Meela amesema utulivu katika sherehe za Krismasi mwaka huu, umechangiwa pia na wananchi kujitambua na kuachana na matukio ya ulevi uliopitiliza ambao umekuwa ukisababisha ajali na vurugu mitaani.

Chanzo: mwananchi.co.tz