Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Arusha waanza kutekeleza agizo la Waziri Lugola, wananchi wafurahia

Sat, 6 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Polisi mkoa wa Arusha wameanza kutekeleza agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kuhusu kutolewa dhamana hadi siku za sikukuu na mapumziko ili kuwasaidia kupunguza mrundikano wa mahabusu katika vituo vya polisi na kurahisisha utoaji wa haki kwa wakati.

Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 4, 2018, Kamanda wa  polisi mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng’azi amesema wamelipokea agizo la Waziri Lugola na tayari limeanza utekelezwaji katika vituo vyote ya polisi mkoa huo.

“Nimekwisha waagiza wakuu wa vituo vyote vya polisi ngazi ya wilaya, kufuata agizo la waziri kwa kutoa dhamana bure siku za sikukuu na mwisho wa wiki kwa watuhumiwa ambao makosa yao yana dhamana” amesema.

Amesema dhamana zote hizo, zitatolewa bila kuvunja kanuni na taratibu za jeshi la polisi hivyo watakaoweza kuzipata dhamana hizo ni wale wenye sifa kwa mujibu wa taratibu na kanuni za polisi.

Mkazi wa Majengo mkoani hapo, Alex Materu alisema analipongeza agizo la Waziri Lugola kwani linawasaidia kwa kuwa kuna makosa mengine ni madogo hayastahili watu kukaa siku nyingi polisi.

Kwa upande wake,  Iddi Shaban mkazi wa Sombetini, amesema jeshi la polisi ni taasisi kubwa na inafanya kazi saa 24 kama hospitali hivyo kadri wanavyozuilia dhamana wanaongeza idadi ya mahabusu na agizo hilo litasaidia kupunguza mrundikano wa mahabusu.

Niksoni Wiliam wa Olasiti jijini Arusha alisema agizo hili litawasaidia kuwatoa ndugu zao kwa wakati na wataondokana na kero za kutozwa fedha wakati wa kuomba dhamana kwa ndugu zao.

Chanzo: mwananchi.co.tz