Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polepole aagiza migogoro ya ardhi kutatuliwa mkoani Kilimanjaro

69154 Pic+polepole

Wed, 31 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Humphrey Polepole amezitaka kamati za ulinzi na usalama Wilaya ya Moshi na Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro na Simanjiro Mkoa wa Manyara kukutana kujadili namna ya kumaliza mgogoro wa wakulima na wafugaji.

Amesema kamati hizo zinatakiwa kukutana Agosti 9, 2019 katika kijiji cha Chemchem ambacho kina mgogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa zaidi ya miaka 10 sasa hali inayotajwa kuchangia uvunjifu wa amani.

Polepole ametoa maelekezo hayo leo Jumatano Julai 31,2019 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chemchem.

“Baada ya kikao cha kamati za ulinzi na usalama Mkoa kukaa mimi nitakuja jioni kwani tunataka tuweke utaratibu mpya hapa. Hatutaki watu waishi kiholela, tunataka waishi kwa amani. Wakulima wafuate taratibu na wafugaji wafuate taratibu. Wote muishi kwa amani na kufuata sheria zilizopo,” amesema Polepole.

Saum Paul, mkazi wa Chemchem  amesema mgogoro huo unatokana na wafugaji kutoka Simanjiro kuingiza makundi makubwa ya mifugo katika mashamba yao na kusababisha athari kubwa.

“Tatizo la mifugo kwenye  mashamba ni la muda mrefu limesababisha hasara kubwa, mwaka jana tuliahidiwa kulipwa fidia lakini hatukulipwa na kwa sasa  tumeshaandaa mashamba lakini hatujui hatma yetu. Ingawa hatujapanda lakini mifugo tayari imeanza kuvuruga mashamba,” amesema Saum.

Pia Soma

Chanzo: mwananchi.co.tz