Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pingamizi la Serikali mwanamke aliyedaiwa kujinyonga mahabusu lakataliwa

Mahabusu Pici Pingamizi la Serikali mwanamke aliyedaiwa kujinyonga mahabusu lakataliwa

Fri, 17 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Korona Kinondoni imeikatalia Serikali hoja zake katika shauri la uchunguzi wa chanzo cha kifo cha mwanamke aliyedaiwa kujinyonga akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Mburahati, Dar es Salaam, Stella Moses, baada ya kutupilia mbali pingamizi lake.

Uamuzi huohuo umetolewa Alhamisi Machi 16, 2023 jioni na Korona, Franco Kiswaga (Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kivukoni (Kinondoni) anayesikiliza shauri la uchunguzi wa kifo hicho lililofunguliwa na familia ya marehemu.

Mahakama ya Korona ni mahakama inayoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo Visivyo vya Kawaida, ili kufanya uchunguzi wa kifo hicho kufuatia shauri la maombi.

Mwenendo wa uchunguzi huo ulitarajiwa kufanyika Machi 9, mwaka huu, Serikali iliweka pingamizi ikipinga Mahakama kuendelea na shauri hilo la familia.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema alieleza kuwa shauri hilo halistahili kuwepo mahakamani kwani lilishaamuriwa kikamilifu na kutolewa amri iliyokuwa inaombwa.

Badala yake alisema kuwa wajibu Serikali imewasilisha mahakamani hapo shauri lake jipya la uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho ambalo ndilo inataka Mahakama ilisikilize badala shauri hilo lililofunguliwa na familia.

Katika uamuzi wake, Kiswaga ametupilia mbali pingamizi hilo, akisema kuwa shauri lililowasilisha na Serikali hata wadaawa hawajajulikana na kwamba kwa kuwa shauri awali tayari wadaawa wanajulikana basi mahakama itaendelea na shauri hilo kufanya uchunguzi huo.

Baada ya uamuzi huo wakili wa familia ya marehemu, Peter Madeleka amefafanua kile ambacho mahakama inapaswa kukifanya kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo Visivyo vya Kawaida, akapendekeza ianzie uchunguzi wa kimahakama katika kituo cha Polisi ambako tukio hilo lilitokea.

Amefafanua kuwa kituoni hapo mahakama itaangalia mazingira ya mahabusu hiyo, kukagua nyaraka zinazotumika kuweka kumbukumbu za mahabusu kituoni hapo, kuangalia kitu kinachodaiwa kutumiwa na marehemu kujinyongea na kuwahoji askari polisi waliokuwa zamu siku hiyo kuna namna gani walitimiza wajibu wao.

Ameongeza kuwa baada ya hapo mahakama itapaswa kwenda makaburini mahali alikozikwa Stela na kwamba kama ikipendezwa kwa kuwa sheria inaipa mamlaka kufukua mwili basi iamuru na mabaki ya mwili wa marehemu yafukuliwe kwa ajili ya uchunguzi wa kipathelojia.

Hata hivyo Wakili wa Serikali Mkuu, Flora Massawe na Mrema wameiomba mahakama iahirishe hatua hiyo ili ipate muda kupitia nyaraka za uchunguzi ambazo wajibu maombi wameziwasilisha wakidai kuwa zina taarifa za uchunguzi na maoni ya wataalamu ambao wanaweza kuisaidia kujua kilichotokea.

Mahakama kuanza uchunguzi kifo cha aliyedaiwa kufia mahabusu

Wakili Madeleka amepinga hoja hiyo ya Serikali pamoja na nyaraka hizo akidai kuwa hazitambuliki kwa kuwa haijulikani zilikotoka na kwamba kama kuna mtu aliyefanya uchunguzi mwingine huko hana mamlaka hayo kwani mwenye mamlaka ya kufanya uchunguzi huo ni korona tu.

Hata hivyo Korona Kiswaga amekubaliana na hoja ya kuahirisha hatua hiyo ili apate muda wa kupitia nyaraka hizo kwanza, huku akiamuru Serikali iwasilishe nyaraka hizo nakala halisi Machi 22 na akapanga kuendelea na shauri hilo Machi 28.

Stella alifariki dunia usiku wa kuamkia Desemba 20 2020, akiwa mahabusu katika kituo cha Polisi Mburahati Dar es Salaam alikojisalimisha baada ya kupata taarifa kuwa alikuwa akihitajika kituoni hapo, kwa madai kuwa alikuwa akidaiwa katika biashara zake za nafaka.

Wawakili wavutana kuhusu mwanamke anayedaiwa kujinyonga mahabusu

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni ilieleza kuwa, taarifa ambayo ilipingwa na familia na ikaomba ufanyike uchunguzi huru kujua chanzo cha kifo chake, bila mafanikio.

Hivyo Machi 2022 shemeji wa marehemu Emmanuel Kagongo, kwa niaba ya familia alifungua shauri la maombi kuomba uchunguzi huo na mahakama ikayakubali maombi hayo.

Wajibu maombi katika shauri hilo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspector General of Police - IGP), Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (DZPC) na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC).

Wengine ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Mburahati (OCD), Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), iliyofanya uchunguzi wa kitabibu wa chanzo cha kifo cha marehemu lakini haikuwahi kutoa taarifa ya matokeo ya uchunguzi huo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live