Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleio ya Makazi Geophrey Pinda ameingilia kati mgogoro wa wananchi kwenye halmashauri ya wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi wanaodai maeneo yao kutwaliwa bila ya kulipwa fidia.
Hatua hiyo ya Pinda inafuatia kupewa malalamiko na Juma Faki Mjaka mkazi wa Kilwa anayedai kutwaliwa eneo lake inapojengwa Bandari ya Kilwa pamoja na familia ya Mwinyimanga inayodai kunyanyaswa kudhulimiwa eneo lao Masoko Pwani wilayani Kilwa.
Naibu Waziri alitembelea eneo inapojengwa Bandari ya Kilwa tarehe 23 Machi 2024 kwa lengo la kujiridhisha madai ya Mjaka na baadaye kukutana na familia ya Mwinyimanga wakati alipokwenda kufungua mkutano wa wadau kuhusu uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika wilaya ya Kilwa.
Baada ya kutembelea eneo inapojengwa Bandari ya Kilwa na kupata maelezo ya mlalamikaji Bw. Mjaka, Pinda aliagiza kuudwa Tume maalum itakayohusisha vyombo mbalimbali ili kubaini ukweli wa malamiko ya mwananchi.
Kwa upande wa familia ya Mwinyimanga inayodai kunyanyaswa na kutwaliwa ardhi yao kwenye eneo la Pwani Masoko katika halmashauri ya Kilwa, Naibu Waziri alitaka makubaliano yanayofikiwa baina ya wanaomiliki ardhi na wale wanaotaka kutwaa eneo kuzingatiwa.