Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limetoa taarifa ya wanandoa kufariki kwa ajali ya pikipiki katika Mlima Kinombedo Mkwiti wilayani Tandahimba.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari leo Jumatatu Desemba 18, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Nikodemus Katembo, amesema kuwa wanandoa hao walipata ajali wakiwa wamepakiana kwenye pikipiki Desemba 17 mwaka huu.
Amewataja wanandoa hao kuwa ni Ismail Chitapwidi (65) na Aisha Bakari Chilambo (55) ambapo walipanda pikipiki aina ya Sanlg.
Amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa mwendesha pikipiki ambaye aliacha njia na kugonga gema upande wa kushoto mwa barabara na kusababisha vifo hapohapo.
Aidha miili ya marehemu ilifanyiwa uchunguzi wa kitabibu katika Hospitali ya Nyangao na baadaye kukabidhiwa ndugu kwaajili ya mazishi.
"Unajua chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa mwendesha pikipiki ambaye aliacha njia na kugonga gema upande wa kushoto mwa barabara na kusababisha vifo hapohapo kwa hili tukio watumiaji wa vyombo vya moto wanapaswa kufuata sheria kanuni na taratibu.
“Jeshi la Polisi linapenda kutoa rai kwa watumiaji wa barabara hususani madereva wa vyombo vya moto kwa ujumla kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwemo kuzingatia kuvaa kofia ngumu (helment) ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika,” Kamanda Katembo.
Kwa upande wake Mratibu wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Kanda ya Kusini Mashariki (RSA), Nassoro Mansour (Babulolo) amesema kuwa waendesha pikipiki wanapaswa kufuata kanuni, taratibu na sheria za usalama barabarani pamoja na zile za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).
“Waendesha pikipiki wanapaswa kuafuata sheria ikiwemo kuvaa kofia ngumu unajua ile ni kazi yao ambayo inaendesha maisha ya watu wengi wanatakiwa kufuata kanuni taratibu na sheria za usalama barabara na zile za LATRA na kuhakiksha wana bima ambayo wakipata ajali wanaweza kufidiwa," amesema Mansour.