Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Petroli yateketeza watano, wanne familia moja

45702 PIC+PETROLI Petroli yateketeza watano, wanne familia moja

Sun, 10 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Same. Ndugu wanne wa familia moja wanaoishi katika kijiji cha Marwa, Kata ya Ruvu wilayani Same wameteketea kwa moto uliotokana na mlipuko wa petroli wakati mmoja wao akimpimia mteja mafuta hayo.

Christina Mndeme (40), muuguzi wa Zahanati ya Marwa aliyekuwa akimpimia mteja mafuta hayo ni miongoni mwa watu watano waliofariki dunia katika tukio hilo lililotokea Jumatano iliyopita saa 1:30 kijijini hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mlipuko wa petroli ambayo ilikuwa jikoni huku shughuli za upishi zikiendelea.

Issah alisema watu wawili bado wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi wakiendelea na matibabu.

Pamoja na Christina wengine waliofariki dunia ni mdogo wake Natujwa Justine (26) na watoto wake wawili ambao ni Jamila Amir (4) na Jonson Rahim (2) huku mtu mwingine akiwa hajafahamika.

Akizungumzia tukio hilo, ofisa uhusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo alisema mpaka sasa kuna majeruhi wawili - mmoja akiwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).

“Tulipokea wagonjwa watano Machi 6, 2019 usiku kutoka Ruvu kwenye tukio la mlipuko wa petroli, mmoja alifariki wakiwa mapokezi na wengine wawili walifariki wakipatiwa matibabu ICU, na sasa wapo wagonjwa wawili ambao madaktari wanaendelea kupambana kuokoa maisha yao,” alisema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Marwa, Elifuraha Masoni alisema mwingine aliyefariki bado hajafahamika na kwamba alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya KCMC.

Alisema katika tukio hilo watoto wawili walifariki papo hapo huku watu watatu wakipoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu KCMC.

Alisema Justine ambaye ni marehemu kwa sasa alikuwa akiishi na dada yake Christina pamoja na watoto wake wawili ambao pia walifariki katika tukio hilo.

Masoni alisema siku ya tukio Christina alikuwa akimpimia mteja wake petroli karibu na jiko la mkaa walilokuwa wakilitumia kupikia chakula jambo lililosababisha mlipuko wa moto.

“Kwa maelezo ya kijana wa Christina ambaye alikuwepo nje ya nyumba wakati tukio linatokea ni kwamba wamekuwa wakifanya biashara ya petroli na siku ya tukio mama yake huyo ambaye ni marehemu alikuwa akimpimia mteja,” alisema mwenyekiti huyo.

“Yusuph Sudi (10), mtoto wa marehemu Christina baada ya petroli kulipuka alipiga kelele kuomba msaada ambapo aliyekuwa mteja aliingia ndani kumuokoa na ndipo na yeye aliposhika moto na kuungua.”

Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule alisema wakati tukio hilo linatokea katika nyumba hiyo kulikuwa na watu saba ambapo watano kati yao walifariki dunia na wawili bado wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.



Chanzo: mwananchi.co.tz