Paroko wa Kanisa la Katoliki, Parokia ya Karatu mkoani Arusha, Pamphili Nada ameuwa kwa kupigwa na kitu kizito na mtu anayedaiwa kuwa na afya ya akili aliyeingia Kanisani kwa nguvu kutaka kusali.
Hata hivyo baada ya mtu huyo aliyejulikana kwa jina la Romani Leonard (30) kufanya mauwaji hayo naye ameuawa na Wananchi wenye hasira.
Kamanda wa polisi mkoa Arusha, Justine Masejo amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo leo Jumatano Julai 19, 2023.
"Padri alifariki wakati anapelekwa hospitali na mtuhumiwa aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya kupata taarifa za tukio hilo,"amesema.
Wakizungumza na mwananchi baadhi ya wakazi wa Karatu walisema mtu huyo, tangu usiku wa kuamkia leo alikuwa anataka kuingia Kanisani lakini walinzi walikuwa wanamzuia.
Rehema Baha amesema hata hivyo alfajiri mtu huyo akiendelea kupiga kelele kutaka kuingia kusali na ndipo Padri Nada alitoka nje na kumwambia mlinzi amfungulie mlango.
"Baada ya kuingia ndani akiwa na Padri tu Kanisani ndipo alichukuwa chuma cha mlango na kumpiga Padri ambaye alifariki akikimbizwa hospitali"amedai shuhuda wa tukio hilo.
Taarifa zaidi za tukio hili tutaendelea kuzitoa fatilia gazeti la Mwananchi na mitandao yake ya kijamii.