Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Panya wanaotafuna viungo vya maiti Gairo wapatiwa dawa

62853 PANYA+PIC

Sat, 15 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Gairo. Wananchi wilayani Gairo mkoani hapa wameondokana na hofu ya panya kunyofoa viungo laini vya maiti nyakati za usiku katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Kituo cha Afya Gairo baada ya Serikali kutoa fedha za kujenga jengo jipya la kuhifadhia maiti.

Akipokea msaada wa vifaa kutoka benki ya NMB juzi, mkuu wa wilaya hiyo, Seriel Mchemba alisema baada ya Serikali kutenga mamilioni ya fedha kwa ajli ya ujenzi wa vituo vipya vya afya na hospitali nchini umesaidia mambo mengi.

Mchemba alisema kabla ya Serikali kupeleka fedha za ujenzi wa kituo kipya hali ilikuwa mbaya, kwani miili ya maiti iliyokuwa inahifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti walikuwa wakinyofolewa viungo vyao laini.

Alisema baada ya kukamilika kwa majengo hayo yatapunguza changamoto nyingi. “Chumba cha zamani cha kuhifadhia maiti kilikuwa chumba cha ajali kwani ilikuwa ukilaza maiti usiku ya mwanaume au mwanamke sehemu nyeti unakuta zimeliwa na panya asubuhi, hata kama watalindwa vipi na nguo,” alisema Mchemba.

Awali, mganga mfawidhi wa kituo hicho, Dk Danstan Mshana alisema kituo kimeongezewa majengo mapya na huduma zimeboreshwa.

Dk Mshana alisema Serikali imeanza kupeleka vifaa tiba vya kisasa ikiwamo mashine ya dawa ya usingizi ambayo ina kazi nyingi kumsaidia mgonjwa.

Pia Soma

“Tulikuwa na tatizo la miili ya maiti kunyofolewa viungo laini kwa wanawake na wanaume nyakati za usiku kutokana na uchakavu wa jengo la kuhifadhia maiti, lakini chumba kipya cha kuhifadhia maiti kitaondoa tatizo hilo,” alisema Dk Mshana.

Naye meneja uhusiano biashara za Serikali Kanda ya Mashariki wa NMB, Anneth Kwayu alisema kituo hicho kimekuwa kikipokea vifaa mbalimbali kwa miaka mitatu mfululizo zikiwa ni jitihada za benki hiyo kusaidia kupunguza changamoto za afya.

Kwayu alisema mwaka huu kituo hicho kimepokea mashuka 62, vitamba vya kulalia wagonjwa vitano na magodoro matano vyenye thamani ya Sh5 milioni.

“NMB imetoa misaada yenye thamani ya zaidi ya Sh400 milioni kwa mwaka huu pekee sekta za elimu,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz