Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pango la ardhi lawatia matatani 50 Morogoro

5e304e9c3c2591ee1e670836807c15f4 Pango la ardhi lawatia matatani 50 Morogoro

Mon, 15 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

OFISI ya Ardhi Mkoa wa Morogoro imeanza kuwabana wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi kwa kuwafikisha wadaiwa sugu 50 wanaodaiwa Sh 1,552,436,750 katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ikiwa ni mkakati wa ofisi hiyo kukusanya madeni na malimbikizo mengine ya ardhi yanayofikia jumla ya Sh trilioni 1.02.

Akizungumza ofisini kwake mwishoni mwa wiki mkoani hapa, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Morogoro, Frank Mizikuntwe alisema wadaiwa waliofikishwa kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ni sehemu ya wadaiwa wa kodi ya ardhi 474.

Alisema hadi fikia Machi 8 mashauri ya wadaiwa hao yatakuwa yamesikilizwa katika baraza hilo na kutolewa uamuzi.

Alisema kati ya wadaiwa 50 waliofikishwa Baraza la Ardhi la Wilaya, 21 ndiyo waliojitokeza kusikiliza mashauri yao ambao kwa kujibu wa Frank walikubali kulipa malimbikizo yao kwa awamu hadi mwisho wa Juni.

“Kwa wadaiwa wasiofika kusikiliza mashauri yao sambamba na watakaoshindwa kukamilisha madeni katika muda waliokubaliana ofisi yangu itasubiri amri ya baraza kwa hatua zaidi ambapo maamuzi yake yanaweza kuwa ni kunadiwa mali za wadaiwa kufidia deni,” alisema.

Alisema Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Morogoro katika kuwafuatilia wadaiwa sugu, imeelekeza nguvu kubwa kwenye halmashauri zenye madeni makubwa ambazo amezitaja kuwa ni Manispaa ya Morogoro Sh trilioni 1.006, Ifakara Sh bilioni 11, Kilosa Sh bilioni 6 na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Sh bilioni 3.8.

"Ofisi yangu imejipanga kuhakikisha inasambaza ilani za madai kwa wadaiwa wote wa kodi za ardhi mkoa wa Morogoro ili tuweze kukusanya kiasi cha fedha kinachodaiwa kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha 2020/ 2021," alisema.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Morogoro, baadhi ya mikakati inayotumika kufuatilia wadaiwa ni kupita katika mitaa kila siku za Jumatatu na Ijumaa na kusambaza hati za madai.

Alisema pia ofisi yake inatoa gari siku moja kwa wiki katika halmashauri kuwawezesha maofisa ardhi kuwafuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi.

Ufuatiliaji wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ni utekelezaji wa Maagizo ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula aliyezitaka ofisi za ardhi za mikoa kuhakikisha wadaiwa wote sugu wanafikishwa kwenye mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya ili walipe madeni kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha 2020/ 2021.

Chanzo: habarileo.co.tz