Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pacha wafariki nyumba ikiungua moto

Pacha Wafariki Pacha wafariki nyumba ikiungua moto

Tue, 1 Aug 2023 Chanzo: Mwananchi

Watoto wawili ambao ni pacha wenye umri wa mwaka mmoja wamefariki dunia baada ya nyumba yao kuteketea kwa moto katika Kijiji cha Magulilwa wilayani Iringa.

Pacha hao, Eliza na Erick Msigwa walipoteza maisha yao kwa nyakati tofauti ambapo mmoja alifia ndani ya nyumba na mwingine wakati akikimbizwa hospitalini kwa ajili ya kutibu majereha ya moto.

Watoto hao waliofariki Julai 30, 2023 na wamezikwa jana Julai 31, 2023 kijijini kwao Magulilwa.

Akizungumza nyumbani kwao, mama wa watoto hao, Warda Msisi amesema kabla ya kufikwa na mauti aliwalaza wanaye ndani ya nyumba hiyo kisha akaenda dukani kununua sabuni.

“Duka lenyewe haliko mbali na sikuchukua muda mrefu, nilipokuwa narudi kwa nilishangaa watu wamekusanyika nyumbani kwangu, nikaona moshi kumbe nyumba inaungua,” amesema na kuongeza;

“Nilishtuka kwa sababu watoto walikuwa ndani lakini nikawa nimechelewa, mmoja alikauka kabisa na mwingine alikuwa bado hai ila aliniacha naye. Sina kingine kinachoniumiza ni hawa watoto tu, sielewi ilikuwaje na sijui chanzo cha moto ni nini hadi sasa”

Baba wa watoto hao Stanley Msigwa, alisema alipata taarifa za nyumba yake kuungua kwa moto wakati akiendelea na kazi zake za kila siku mbali na nyumbani kwake.

“Kuna watu waliniambia nyumba yangu inaungua lakini nikabisha kwa sababu ni ya bati, niliwaza inaunguaje? Wakasema ni kweli hivyo nikatoka mbio kuja na kuona ni kweli. Kilichoniumiza zaidi ni wanangu, mmoja alipookolewa nilijua anaweza kusalimika lakini naye akafariki,” alisema.

Alisema mbali na wanaye kupoteza maisha hakuna kitu walichoweza kuokoa ikiwamo nguo, vyombo na chakula.

“Kama unavyotuona, nguo ndio hizi hizi tulizovaa kila kitu kimeungua. Wanangu walikuwa wanaanza kutembea na walikuwa bado wananyonya,” amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Magulilwa, Stephan Madege alisema tukio hilo limewasikitisha hasa kitendo cha watoto hao kuteketea kwa moto.

“Ni tukio ambalo limetuumiza kama kijiji, tumeshawazika hawa watoto na polisi walituamba wanaendelea na taratibu zao za kufanya uchunguzi kujua chanzo cha moto. Nitoe pole kwa wazazi, ndugu jamaa na marafiki,” amesema Madege.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi zaidi.

Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jakson Kiswaga aliwataka watu watakaoguswa na tukio hilo kuichagia familia hiyo ambayo licha ya kuondokewa na watoto, imepoteza vitu mbalimbali ikiwamo nguo.

Chanzo: Mwananchi