MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imetoa msaada wa mifuko 200 ya saruji kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha Huruma Center cha mjini Iringa itakayotumika kusaidia ujenzi wake wa shule msingi.
Kituo hicho kinajenga shule hiyo itakayotoa fursa ya elimu watoto hao yatima wakiwemo waliofanyiwa ukatili ukiwemo ubakaji na ulawiti na kupelekea wakimbie majumbani mwao kwa ajili ya kulinda usalama wao.
Akikabidhi mifuko hiyo ya saruji mbele ya viongozi wa kituo,dini na serikali, Mkurugenzi wa Tehama kutoka PPRA Michael Moshiro alisema wametoa msaada huo ili kuunga mkono juhudi za wadau mbalimbali zinazolenga kuwapa fursa ya elimu watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Ujenzi wa shule hiyo umefikia hatua ya kupaua katika jengo la awali ambalo litagharimu jumla ya Sh Milioni 185.
Mlezi wa kituo hicho Mchungaji Joyce Ngandango amesema kukamilika kwa shule ya Huruma kutawasaidia watoto hao kutoka katika hatari ya kukosa fursa ya elimu kwasababu ya athari za kisaikolojia walizokutana nazo baada ya kufanyiwa ukatili.
“Tunao watoto ambao kesi zao ni nyeti wengine wanahitajika kwenda kutoa ushahidi mahakamani hivyo tunawatunza kwa usiri na hawatakiwi kutoka nje ya kituo, hawa wanakosa fursa ya kwenda shule hadi kesi zimalizike,” alisema.
Akizungumza kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Venonica Kessy amewashukurua PPRA kwa mchango huo akisema utasaidia kuharakisha ujenzi wa shule hiyo.
Mbali na mifuko hiyo 200 ya saruji, watumishi wa PPRA wametoa misaada mbalimbali katika kituo hicho ikiwemo mablenketi 45, mashuka 90, vyandarua 45, vifaa vya usafi, mafuta ya kupaka, counter book dazani 10, mchele kilo 100, mafuta lita 40 na unga wa ngano kilo 100.
Kituo cha kulelea watoto cha Huruma kwasasa kina watoto 81 na tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994 kimehudumia watoto zaidi ya 800.