Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

PIC yaiagiza Serikali kupeleka Sh1.9 bilioni mradi wa maji Nzuguni

Kero Majipic PIC yaiagiza Serikali kupeleka Sh1.9 bilioni mradi wa maji Nzuguni

Mon, 29 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mitaji ya Umma na Uwekezaji (PIC), imeiagiza Serikali kutoa Sh1.9 bilioni ili kukamilisha mradi wa maji wa Nzuguni jijini Dodoma, uliotakiwa kukamilika Januari 15, 2024.

Jiji la Dodoma lina upungufu wa maji wa nusu ya mahitaji ambapo mahitaji kwa siku ni lita milioni 133, lakini zinazozalishwa ni lita milioni 68.8, hali inayoifanya huduma hiyo kutolewa kwa mgawo.

Kukamilika kwa mradi wa Nzuguni kutaongezeka uzalishaji kwa asilimia 11.7 na kunufaisha wakazi 75,968 wa maeneo ya Nzuguni, Swaswa, Ilazo na Kisasa jijini Dodoma.

New Content Item (1)

Akizungumza leo Jumapili, Januari 28,2024 alipotembelea mradi huo unaondeshwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma, Mwenyekiti wa PIC, Deus Sangu amesema watakwenda kuzungumza na Serikali ili kutatua changamoto hiyo.

“Tunaona fedha zilizolipwa kwenye mradi huo ni Sh3.3 bilioni. Hapa kuna fedha wanazodaiwa (Serikali) ilitakiwa mradi huu ukamilike Januari 15, mwaka huu lakini umeshindwa kukamilika kwa sababu fedha hazijaja kama ilivyotakiwa,”amesema.

Amesema wao kama kamati wanalibeba jambo hilo na kwenda kutoa msukumo kwa Serikali wakamilishe ulipaji wa fedha, ili wakandarasi wakamilishe kazi na wananchi wapate maji.

Mwenyekiti huyo amesema kamati hiyo inapigania kuhakikisha mamlaka za maji zinakuwa na uwezo wa kufuatilia hasa upotevu wa maji kwa sababu maji mengi yanayozalishwa na mamlaka yamekuwa yakipotea.

Sangu ambaye pia ni mbunge wa Kwela, amesema wakati mwingine hata namna ya kujua kiasi cha maji kinachopotea imekuwa ni changamoto.

Hata hivyo, amesema kwa kutumia mfumo wa Tehama, changamoto hiyo itatatulika na kuzitaka mamlaka nyingine za maji kutembelea Duwasa, ili kujifunza jinsi walivyotekeleza jambo hilo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa, Aron Joseph amesema Sh3 bilioni sawa na asilimia 71, zimeshalipwa na Serikali katika mradi huo na mamlaka yake wamebana Sh500 milioni kutoka maeneo mengine ili utekelezaji wake usikwame.

“Tuna upungufu wa kama Sh1.9 bilioni kwa ajili ya kukamilisha na kasi (utekelezaji) imepungua kidogo. Naamini hili (kamati) mtalichukua ili tukamilishe mradi huu kwa asilimia 100. Mradi huu ulikuwa ukamilike Januari 15, 2024 lakini kwa changamoto hizi za fedha kidogo tumepunguza kasi,” amesema.

Joseph amesema mradi huo ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 96, utawahudumia wakazi 75,668 na kuwa utaongeza uzalishaji wa maji kutoka asilimia 50 hadi asilimia 61.7.

Naye diwani wa Nzuguni, Aloyce Luhega ameomba mamlaka hiyo kusambaza mtandao wa maji katika kata yake ambao ni chakavu na hivyo kusababisha mabomba kupasuka kutokana na kasi ya maji.

Katibu wa Mwenezi wa Mkoa wa Dodoma, Jawadu Mohamed amesema chama hicho kitahakikisha kila nyumba ya mkazi wa jiji hilo inapata maji kwa sababu wanamini huduma hiyo ndiyo ahadi kuu, uhai na ni siasa

Chanzo: www.tanzaniaweb.live